Mbunge wa Kisesa, Luhaga Mpina
MBUNGE wa Kisesa, Luhaga Mpina, ameibana Serikali bungeni, kuhusu hatma ya kesi 1,097 za malimbikizo ya kodi yenye thamani ya Sh. 360 trilioni na dola za Marekani 181.4 milioni, ambazo hazijatolewa maamuzi. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma…(endelea).
Mpina amehoji hayo bungeni jijini Dodoma, leo Alhamisi, tarehe 22 Septemba 2022.
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Hamad Chande, amesema hadi kufikia Agosti 2022, kulikuwa na mashauri 854 yenye kodi inayobishaniwa kiasi cha Sh. 4.21 trilioni na dola za Marekani 3.48 milioni, kwenye hatua mbalimbali za usikilizaji katika taasisi za rufani za kodi.
Dk. Mwigulu
Hata hivyo, Mpina hakuridhika na majibu hayo kutokana na kuwa tofauti na swali alilouliza hususan katika idadi ya mashauri na thamani yake.
Huku akiibana Serikali kwa kuihoji kwa nini ilikubali kupokea Sh. 700 bilioni badala ya Sh. 360 trilioni, fedha za malimbikizo ya kodi ambazo ilikuwa inazidai kampuni za madini.
“Kwanza nisikitike kwamba swali limeulizwa trilioni 360, lakini limejibiwa trilioni 4.21. Hata hivyo, ninayo maswali ya nyongeza, la kwanza kwa nini Serikali iliamua kukubali kupokea Sh. 700 bilioni kutoka katika malimbikizo ya makampuni ya madini maarufu makinikia badala ya trilioni 360 ambayo ni madai halali katika nchi yetu,” alihoji Mpina.
Pia, Mpina alihoji nini kilichoifanya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), ishindwe kukusanya malimbikizo ya kodi yasiyo na kesi ya Sh. 7.54 trilioni na kusababisha ongezeko la malimbikizo ya kodi kufikia asilimia 94.6.
Baada ya Mpina kuonesha kutoridhishwa na majibu hayo, Waziri wa Fedha na Mipangoi, Dk. Mwigulu Nchemba, aliinuka na kutoa ufafanuzi akisema kesi za malimbikizo ya kodi zinazosikilizwa katika taasisi za rufaa za kikodi zina thamani ya Sh. 4.21 trilioni, badala ya Sh. 360 trilioni alizosema Mpina.
“Hizi trilioni 360 haziko kwenye mashauri ya kikodi, kwa hiyo hayapo kwenye rufaa za kikodi. Hili ni jambo mahususi ambalo lilikuwepo kwenye mzozo wa Serikali pamoja na Barrick, kwa hiyo ni kitu tofauti,” amesema Mwigulu.
Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson
Kuhusu swali lililohoji kwa nini Serikali ilikubali kupokea Sh. 700 bilioni, badala ya Sh. 360 trilioni za malimbikizo ya kodi katika kampuni za madini maarufu kama makinikia, Mwigulu alisema Serikali haikuchukua uamuzi huo kimya kimya, bali iliweka wazi sababu ilizofanya izipokee.
“Spika kwenye swali la msingi la Sh. 360 trilioni, Serikali haijapokea kimya kimya, haijakubali tu kupokea fedha hizo kwa maana ya kuacha Sh. 360 trilioni, isipokuwa kilichofanyika Serikali ilipeleka malalamiko dhidi ya makampuni haya ya madini na baada ya malalamiko kupelekwa….,” amesema Mwigulu.
Kutokana na ufafanuzi wa Dk. Mwigulu, Spika wa Bunge, Tulia Ackson, alimtaka Chande alijibu upya swali la msingi la Mpina, kama lilivyoulizwa.
“Mimi nimekuelewa, yeye aliuliza swali tofauti, sasa hayo majibu ndiyo yajibiwe kwenye maswali yake kwa sababu ndicho alichouliza, kama hakipo ajibiwe hakipo, kama hakipo msilete kingine. Naibu Waziri swali lake la msingi liletwe majibu kama lipo, na kama halipo mseme halipo. Ninyi mleteeni majibu kadiri alivyouliza swali lake,” amesema Spika Tulia.
Sakata la makinikia liibuka mwaka 2017, baada ya Serikali kuzuia makontena zaidi ya 200 katika Bandari ya Dar es Salaam, yaliyokuwa na mchanga wa dhahabu. Serikali ilizuia makontena hayo yaliyokuwa katika hatua za kusafirishwa nje ya nchi, hadi wamiliki wake walipe malimbikizo ya kodi waliyokuwa wanadaiwa.
Mnamo 2020, Serikali ilitoa kibali cha makontena hayo kusafirishwa nje ya nchi, baada ya wamiliki wake Kampuni ya Barrick Gold-Corp ya nchini Canada, kukubali kulipa malimbikizo ya kodi ya Sh. 694 bilioni, pamoja na kusaini makubaliano ya kuanzisha kampuni ya madini kati yake na Serikali.
Mwanahalisi