Mti wa Mbuyu Ulivyoua Wapenzi Kikatili



WATU wawili ambao ni wapenzi wamefariki dunia baada ya tawi kubwa la mbuyu kukatika na kuiangukia nyumba yenye vyumba vitano waliyokuwa wamelala eneo la Mkwajuni wilayani Kinondoni mkoani Dar es Salaam usiku wa kuamkia jana.

Mti wa mbuyu ukiwa umeangukia nyumba yenye vyumba vitano, Mkunguni A, Kinondoni Mkwajuni mkoani Dar es Salaam juzi usiku na kusababisha vifo vya watu wawili. 

jioni walimwona kwa mara ya kwanza akifika kwa jirani yao huyo na saa chache kukumbwa na baa hilo.

Tukio hilo la kusikitisha lilitokea majira ya 5:30 usiku kwenye nyumba hiyo iliyoko kwenye kingo za Bonde la Mto Msimbazi, pembeni mwa Barabara ya Kawawa.

Nyumba hiyo iko mita chache kutoka Kituo cha Daladala cha Mkwajuni kuelekea Magomeni, ikiwa ni miongoni mwa nyumba chache zilizosalia baada ya bomoabomoa iliyowakumba watu waliokuwa wanaishi bondeni mkoani Dar es Salaam.

Akizungumza na Nipashe jana eneo la tukio, Hamida Mtilwa, mmiliki wa nyumba hiyo ambayo Asha alikuwa mpangaji wake katika chumba kilichoangukiwa na tawi la mbuyu, alisema tukio hilo lilitokea wakati ambao wote walikuwa wamelala.


“Nyumba hii ina vyumba vitano, tuliokuwa ndani ni watu watano yaani mimi, mtoto wangu mwenye umri wa miaka 13 ambaye anasoma darasa la saba, kaka yangu ambaye alikuja kunitembelea na mpangaji wangu, Asha na mpenzi wake,” alisimulia.

'Mama mwenye nyumba' huyo (Hamida) alisema kuwa akiwa chumbani kwake, ghafla alishtuka baada ya kusikia kishindo kikubwa na alipoamka, aliona bati la chumba chake likiwa limetumbukia ndani na matofali yamebomoka.

“Nilipokwenda nje, nikakuta mbuyu umeshadondoka, umeangukia chumba cha mpangaji wangu Asha ambaye ndani alikuwa amelala na mpenzi wake ambaye alinitambulisha jana (juzi) jioni baada ya kuja naye hapa kuwa ni mpenzi wake, huyu kijana simfahamu, ni mara yake ya kwanza kuja hapa," alisimulia.


Aliendelea kubainisha kuwa Asha amekaa kwenye nyumba hiyo kama mpangaji kwa karibu miezi mitano na alikuwa akilipa Sh. 25,000 kodi ya chumba kwa mwezi.

“Huyu mwanaume ninaona watakuwa wanalingana, siyo mkubwa sana, tunaiomba serikali itusaidie kwa sababu mti huu umedondoka sehemu na mwingine umebaki (matawi mawili yamebaki), waje kuukata wote ili usiendelee kuleta maafa kwa sababu kama unavyoona hapa, kuna nyumba zaidi ya tatu zimeuzunguka huu mbuyu,” alisema huku akionyesha mazingira yaliyoko huko.

Hamida alisema katika tukio hilo, chumba kimoja kimebomoka kabisa na vingine vilivyobaki ambavyo ni vinne, vimeathiriwa kwa kiasi kikubwa na mti huo.

“Nimeambiwa na viongozi waliofika hapa leo (jana) asubuhi kwa ajili ya usalama wetu tusilale humu ndani, kama unavyoona mwenyewe baadhi ya vyumba matofali yameanguka, mtoto wangu amepata michubuko mwilini,” alisema.


Hamida alibainisha kuwa mpaka wakati huo, kitu pekee ambacho alikuwa ameokoa ni yeye na mwanawe lakini vitu vingine vyote vipo ndani ya nyumba hiyo na wamelazimika kuweka ulinzi nje ya nyumba hiyo.

“Ninawaomba Watanzania wenzangu kutokana na changamoto iliyonipata na kwa sasa sina pa kulala na mtoto wangu, na mimi shughuli zangu kubwa ni uokotaji wa chupa mtaani, ninaomba msaada wa fedha za kujikimu kwa kipindi hiki kigumu ninachopitia,” Hamida aliomba msaada na kutaja namba zake za simu ambazo ni 0659 627434.

Shuhuda wa tukio hilo, William Laurence anayeishi jirani na nyumba hiyo iliyoangukiwa na tawi la mbuyu, alisema kuwa juzi jioni akiwa ameketi chini ya mti huo, Asha alifika huko akitokea kwenye mihangaiko yake.

“Tulikaa hapo mpaka saa moja hivi usiku, akashuka huku chini (eneo la Bonde la Mto Msimbazi), akawa anaongea na vijana waliokuwapo wakati huo, baadaye akapandisha juu na kurudi na kijana (marehemu) ambaye ndiyo kwa mara ya kwanza ninamwona, akanitambulisha kuwa ni mpenzi wake.


“Akamtambulisha na mama mwenye nyumba wake (Hamida) kuwa ‘huyu ni mume wangu’, basi baadaye nikaondoka kwenda nyumbani na mama mwenye nyumba alikuja akaangalia TV nyumbani kwetu, baadaye akaondoka kwenda kulala.

"Nikiwa ndani, nikawa ninaona kama ardhi inatikisika na nje nikawa ninasikia kishindo, nikajua labda gari limefeli breki,” alisimulia.

Laurence alisema wakati anatoka ndani kwake kwenda nje kushuhudia alichokihisi, alikutana na dada yake mlangoni akamrudisha ndani na kumwambia mti unadondoka.

“Baada ya mti kuanguka tulipokuja hapa tukakuta chumba cha mpangaji ndiyo kimedondokewa na mti, tukaanza kuwatafuta kwenye kifusi cha nyumba na kumkuta Asha na huyo kijana wakiwa kwenye godoro lakini mwanamke alikuwa bado hajafa, ila yule mwanamume alikuwa ameshafariki dunia.

“Kaka wa mama mwenye nyumba akafanya utaratibu akamchukua Asha na kumpeleka Hospitali ya Magomeni na baadaye Hospitali ya Mwananyamala, alitupigia simu kuwa amefariki dunia, polisi walifika wakauchukua mwili wa yule kijana na kuupeleka Mwananyamala,” alisema.


Mjumbe wa Serikali ya Mtaa wa Kinondoni Mkwajuni Mkunguni A, Rashid Seleman, alisema kuwa baada ya tukio hilo, waliomba msaada polisi ambao walifika usiku huo na kuchukua mwili.

Alisema Mbunge wa Kinondoni, Abbas Tarimba, pia alifika eneo hilo na kuwaeleza kuwa kwa sababu sehemu ya mti huo bado haijadondoka, waangalie uwezekano wa kukatwa.

“Wamekuja wataalamu wa misitu hapa kuangalia namna ya kuuondoa, wamesema wapo tayari muda wowote kuuondoa lakini changamoto ikaja kuna nyumba kama mbili zitaathirika wakati wa kuuondoa, kuna nyumba moja ina chumba na choo na nyingine yenye vyumba vitatu,” alisema.

Katibu wa Afya Hospitali ya Rufani ya Mkoa Mwananyamala, Rajabu Kaseke, alipotafutwa na Nipashe jana, alikiri kupokea miili ya watu hao, akiwa na ufafanuzi kwamba wote wawili walipokewa hospitalini huko jana wakiwa ni wafu.

Katika ufafanuzi wake kwa Nipashe, Kaseke alisema miili iliyopokewa ni ya Asha Baruani (36) na dereva Charles Nelson (36), yote imetambuliwa na ndugu zao.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad