Familia ya kijana Yahaya Aboubakar, aliyeuawa mikononi mwa polisi yaomba haki itendeke kwa waliohusika na mauaji hayo.
Kijana Yahaya Aboubakar mwenye umri wa miaka 15 anadaiwa kukamatwa na askari polisi nyumbani kwa bibi yake mtaa wa Juhudi, Kata ya Mabatini wilaya ya Nyamagana Septemba 2, 2022, akiwa mzima, kisha polisi hao waliondoka nae na kumfungia ndani bibi yake Yahaya ambapo baada ya kufanikiwa kutoka ndani alifanya jitihada za kumtafuta mjukuu wake katika vituo vya polisi na kumkosa.
"Wakasema wewe mama fungua nikawauliza nyie kina nani? mna kibali cha kuingia humu wakasema wao ni maaskari mbona hakuna mwenyekiti wala balozi wakasema ukigoma kufungua tunapiga mawe, baadae saa kumi na mbli marehemu akafika mjukuu wangu akawekewa mtutu huku na huku akaambiwa fungua mlango akafungua mlango wakamshika wakamuweka chini marehemu akalalamika akasema msinipige mimi sijabisha mnipeleke tu kama ni kituoni mimi nikamwambia mtoto huyo ni mgonjwa msimpige mpelekeni tu tutamfuatilia" ameeleza Bibi wa marehemu.
Mama mzazi wa Yahaya, Rehema Simba, amesema baada ya kuzunguka vituo vyote vya polisi kikiwemo kituo kikuu cha Nyamagana na kumkosa kijana wake ndipo akakutana na mkuu wa upelelezi akamwambia aende kwa RCO ili amueleze mtoto wake alipo.
"Baada ya kufika kwa RCO akasema shida nini nikamuelezea kwamba tumekuja ofisini kwako kuna kijana wangu amekamatwa tumeshazunguka vituo vyote vya polisi hatujampata akasema mtoto wako yupo Bugando Mochwari nikamuuliza mochwari amefuata nini? mbona mapolisi walimchukua nyumbani akiwa mzima? akaniambia kwamba baada ya kuchukuliwa na polisi alipelekwa eneo la mashiri na kupigwa na wananchi ndipo akafariki," ameeleza mama wa marehemu.
Ramadhan Ng’anzi ni Kamanda wa Polisi mkoa wa Mwanza, amesema bado uchunguzi unafanyika wa tukio hilo na atakayebainika kuhusika na mauaji hayo atachukuliwa hatua za kisheria.