Barua iliyoachwa na mwanafunzi aliyekatisha uhai wake, imefichua sintofahamu ya tukio hilo baada ya kubainika binti huyo alijinyonga kutokana na tuhuma alizopewa za kuiba penseli ya mwanafunzi mwenzake.
Msichana huyo, Fransisca Dokee (16), anadaiwa kujinyonga katika moja ya mabweni ya shule hiyo baada ya Naibu Mkuu wa Shule ya Wasichana ya Tala iliyopo Kaunti ya Machakos, kumtaka arejeshee vitu alivyodaiwa kuiba.
Ripoti ya Agosti 31, 2022 iliyotolewa na mkuu wa shule hiyo na naibu wake katika Kituo cha Polisi cha Tala ilisema, “Naibu mkuu wa shule alikuwa akishughulikia suala la mwanafunzi wa kidato cha tatu(16), la kuiba Shilingi 2,500 na boksi la penseli.
Barua iliyoandikwa na Mwanafunzi Fransisca Dokee (16), aliyejiuwa akituhumiwa kuiba penseli.
Kulingana na uongozi wa shule hiyo, umesema mwanafunzi huyo ‘alikubali’ kurejesha vitu vilivyotajwa na kisha inasemekana aliambiwa amtafute mkuu wa bweni ambaye alitakiwa kumpatia funguo za kumwezesha kuchukua vitu hivyo.
Ripoti hiyo imesema, “Mwanafunzi alichukua muda mrefu sana kurudi, hivyo kumfanya naibu mkuu wa shule kuwa na shaka na alikwenda bwenini akiwa na wanafunzi wengine watatu na kukuta mwanafunzi akiwa tayari amejinyonga.”
Baadaye, Polisi waliitwa eneo la tukio ili kuanza uchunguzi na mwili wa mwanafunzi huyo ulipelekwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya Kangundo, huku mama wa marehemu akiushutumu uomgozi wa shule hiyo kwa kushindwa kumudu tukio zima tangu awali.
Katika barua hiyo, ambayo alimuandikia mama yake mwanafunzi huyo hakutaja kiasi cha Shilingi 2,500 anazodaiwa kuiba bali alizungumzia tuhuma za wizi wa penseli pekee huku akidai hakupewa nafasi ya kujieleza.
“Niliwaambia sihusiki na penseli zilizopotea lakini hamkuniamini mkasisitiza mimi ndiye, kweli Mungu pekee ndiye anayejua lakini kwa kuwa sitaki kuleta shida zaidi katika shule hii na kumwacha mama yangu ateseke tena kwa sababu yangu, niruhusuni nitoke,” ilisema sehemu ya barua hiyo.
Aidha, barua hiyo ilizidi kutoa maelekezo kuwa, “Mungu akubariki kwa kunitia moyo daima bye bye ila nitakuja kukutana nawe, baba, na ninaomba usimshirikishe mama yangu katika hili kwa sababu bado ana kazi za kufanya kwa ajili ya ndugu zangu.”