Mwanafunzi wa kidato cha tatu katika Kaunti Ndogo ya Marakwet Magharibi ameingia mitini baada ya kuchoma nyumba ya familia kutokana na kutofautiana na babake kuhusu pesa za matumizi ya shuleni ambazo alimpatia.
Mwanafunzi huyo alikataa Sh1000 za matumizi alizopewa na baba yake, Jacob Kilimo akidai Sh 2000 ambazo mzazi huyo alikataa kumpatia kwa madai kuwa wapo ndugu wengine ambao walipaswa kwenda shule na pia wanahitaji usafiri wa mfukoni na karo ya shule.
Akithibitisha kisa hicho, Chifu wa lokesheni ya Koibirir Allan Cheserek, alisema kuwa mvulana huyo ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha tatu katika Shule ya Sekondari ya Wavulana ya Kapcherop alisema kuwa ndugu zake wengine hawapaswi kupata mengi kwa vile wao ni wasomi wa kutwa.
Madai yake yalipokataliwa kuzingatiwa aliamua kuteketeza nyumba ya familia na ghala akiharibu mali ya thamani isiyojulikana kabla ya kukimbia.