Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Geita, linamshikilia Shelida Ibrahim (20), Mkazi wa Mtaa wa Mkoani Halmashauri ya Mji Geita, kwa kosa la kuwapigia simu zimamoto na kuwaambia kuna tukio la moto na baadaye akazima simu yake kwa lengo la kujifurahisha.
Afisa wa Jeshi hilo Inspekta Edward Lukuba amesema Shelida baada ya kutoa taarifa hiyo alisababisha Jeshi hilo liingie hasara ya kuwasha magari na kukimbilia eneo ambalo walidanganywa.
"Leo tumegundua anaitwa Asia au Shelida lakini jana alijitambulisha kama Rehema Mwiti, alipiga simu kwa hisia nyumba inaungua, Askari walitoka baada ya kukaribia yule Dada alizima simu, hakupatikana tena, leo Septemba 6 kupitia Askari wetu tuliweza kumbaini na kumnasa tumefanya nae mahojiano na amekiri hilo kwamba anafanya hivyo kwa kujifurahisha"
Lukuba amesema kwa mwezi kumekuwa na wastani wa matukio ya uongo matano.
Kwa upande wake Mtuhumiwa wa tukio hilo ameomba radhi kwa kudanganya “Nilipiga simu kwa Jeshi la Zimamoto niliwatumia taarifa za uongo baada ya hapo walivyotaka maelekezo ili waje mahali nilipo nikazima simu, asubuhi wakanikamata, mwenye tabia hii chafu na wanaoshindwa kutumia simu zao vizuri, nilikuwa naomba msirudie”