Namuona Mwai Kibaki Ndani ya William Ruto Kenya


Dar es Salaam. “Wakenya wameamua kuukataa ukabila kwenye Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9, 2022 kwa kuchagua kiongozi wamtakae. Sitauvunja upinzani kwenye Serikali yangu kwa kufanya maridhiano bali nitauacha ushamiri ili kuleta uwajibikaji katika serikalini.” Ni kauli ya Rais wa Kenya, William Ruto, wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye ukumbi wa Bomas baada ya kutangazwa na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ya Kenya kuwa mshindi wa uchaguzi huo.

Ruto aliyeibuka mshindi kwenye uchaguzi huo kwa idadi ya kura milioni 7.1 huku akimuacha mpinzani wake wa karibu Raila Odinga aliyepata kura milioni 6.9 ikiwa ni tofauti ya takribani kura 200,000 tu, mazingira yake ya kuingia madarakani yamefanana kwa ukaribu na yale yaliyomuingiza madarakani Rais wa awamu ya tatu wa nchi hiyo Mwai Kibaki kwenye uchaguzi wa mwaka 2002.

Kwenye uchaguzi wa mwaka 2002, Rais aliyekuwa anamaliza muda wake kwa kipindi hicho, Daniel Moi, alikuwa anamuunga mkono mgombea wa tiketi ya chama cha KANU, Uhuru Kenyatta huku mshindani wake akiwa Mwai kibaki aliyegombea kwa tiketi ya muungano wa National Rainbow akiibuka mshindi kwa kura milioni 3.6 ambayo ilikuwa ni sawa na asilimia 61.3 ya wapiga kura wote wa nchiyo kwa kipindi hicho. Hali hii ni sawa na uchaguzi wa mwaka huu ambao mgombea aliyepigiwa chapuo na Rais anayetoka madarakani (Raila Odinga) hakushinda kwenye kinyang’anyiro hicho.

Pengine tukio la mgombea anayeungwa mkono na Rais anayemaliza muda wake nchini Kenya kushindwa kwenye uchaguzi kwa mara ya pili inaweza kufananishwa na moja kati ya falsafa za kisiasa inayoitwa ‘Sympathy with inferior’ yaani hali ya kumuonea huruma mtu asiyeungwa mkono na watu wenye nguvu kwenye siasa ambaye mara nyingi huonekana ni dhaifu na hupewa nafasi ndogo ya kushinda.

Jambo lingine linalonifanya niwafananishe viongozi hawa wawili ni wadhifa ambao wamewahi kuhudumu kabla ya kushika nafasi ya urais ambayo ni kubwa Zaidi nnchini humo, hawa wote wamewahi kushika nafasi ya umakamu Rais wa nchi hiyo, Kibaki alikamata nafasi hiyo kwa miaka 10 kuanzia 1978 hadi 1988 chini ya Rais Moi kabla ya kutimkia upande wa upinzani kisha kuwa Rais, sawa na Ruto ambaye amekuwa makamu wa Rais kuanzia 2013 hadi 2022 chini Rais Uhuru Kenyatta huku mwishoni mwa uongozi wao, Ruto alifungua chama cha upinzani cha UDA ambacho kilimemuingiza madarakani na kiuwa Rais.

Endapo Ruto ataendelea kuziishi kauli alizozitoa baada ya kutangazwa kuwa mshindi wa kiti hicho, hasa ile ya kuimarisha upinzani nchini humo ili kuongeza uwajibikaji moja kwa moja atakuwa anaendana na Rais Kibaki ambaye wakati wa utawala wake aliwaacha wapinzani wakosoe lakini pia anatajwa kuwa Rais ambaye hakuutaka umaarufu kitu kilichomfanya mara nyingi asijitokeze hadharani kama ilivyokuwa kwa Rais aliyemfuata (Uhuru Kenyatta). Hivi sasa ni miongo miwili imepita tangu Kibaki aingie madarakani kwa kumshinda mgombea aliyenadiwa kwa nguvu zote na Rais aliyekuwepo madarakani wakati huo, tunakuja kumpata mtu mwingine kama Kibaki anayeshinda katika mazingira sawa na yale ya kibaki ila akiwa na mtihani wa je, ataweza kuuishi utulivu wa kisiasa kama aliouishi Mwai Kibaki?

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad