YANGA imemtambulisha rasmi Andre Mtine, raia wa Zambia kuwa Ofisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa Klabu hiyo kwa mkataba wa miaka miwili.
Akizungumza mara baada ya kutambulishwa leo jijini Dar es Salaam, mtendaji huyo ameahidi kufanya kazi kwa bidii na kuipatia klabu hiyo mafanikio kitaifa na kimataifa.
“Ninaamini kwa kufanya kazi pamoja na Rais Hersi Said na wajumbe wa Kamati ya Utendaji (EXCOM), tutafanya mambo mengi makubwa kwa manufaa ya klabu,” anasema.
Aliwapongeza mashabiki wa Yanga na kusema kuwa mchango wao ni mkubwa katika kuifikisha klabu hiyo katika mafanikio.
“Pongezi kwa mashabiki wa Yanga, bila wao klabu isingekuwepo hapa leo. Ni faraja kuona Yanga ina mashabiki wengi wanaoiunga mkono nchini nzima, bila ya mashabiki hawa kusukuma timu mbele, Yanga isingefika hapa ilipofika leo,” alisema.
Awali akizungumza katika hafla hiyo ya utambulisho, Rais wa Yanga, Hersi Said, alisema uteuzi wa mtendaji huyo mpya ulipita katika mchakato wenye uadilifu mkubwa.
Zambia anakotoka mtendaji huyo mpya, ndiko anakotoka kiungo mahiri wa Simba ya Dar es Salaam, Clatous Chama ‘Mwamba wa Lusaka’, pamoja na Mosses Phiri ambaye ametokea kuwa mfungaji mahiri wa Simba katika muda mfupi aliojiunga na timu hiyo