Moshi. Ni mwisho wa James Mbatia NCCR-Mageuzi? Hili ndilo swali wanalojiuliza wengi baada ya chama cha NCCR-Mageuzi kuitisha mkutano mkuu jijini Dodoma wiki ijayo, lengo likiwa ni kumweka kiti moto Mbatia, aliyesimamishwa Mei 21, mwaka huu.
Kwa miezi kadhaa sasa, chama hicho kimekumbwa na mgogoro uliokigawa makundi mawili, moja linaloungwa mkono na Mwenyekiti Mbatia, la pili ni lile linaloungwa mkono na Katibu Mkuu wake, Martha Chiomba.
Kundi hilo la Martha linalomhusisha pia Mwenyekiti mpya wa Baraza la Wadhamini wa NCCR-Mageuzi, Joseph Selasini ndilo linaloonekana kuwa na nguvu kubwa na baraka za Ofisi ya Msajili wa vyama vya Siasa nchini Tanzania.
Hii inathibitishwa na ukweli kuwa kikao cha Halmashauri Kuu ya NCCR-Mageuzi cha Mei 21, mwaka huu kilichomsimamisha uongozi Mbatia na Makamu Mwenyekiti wake Tanzania Bara, Angelina Mtahiwa, kilihudhuriwa na Naibu Msajili, Sisty Nyahoza na alikitambua.
Kikao hicho kilifikia maamuzi hayo kikieleza tuhuma mbalimbali kuwa ni pamoja na utendaji usioridhisha, kugombanisha viongozi, kulazimisha viongozi kujiuzulu na kukosa uaminifu, pia kikao hicho kilivunja Baraza la Wadhamini.
Kwa hali ilivyo na kwa kuwa kundi hilo ndio limeitisha mkutano mkuu, uwezekano wa Mbatia kuvuka kiunzi hicho ni mdogo na tayari mitandao ya kijamii inabashiri huenda mkutano huo ukafunga kitabu cha Mbatia ndani ya NCCR-Mageuzi.
Akizungumza na gazeti hili jana, Selasini, ambaye pia ni mjumbe wa Halmashauri Kuu ya NCCR-Mageuzi alilithibitishia gazeti hili kuitishwa kwa mkutano huo.
“Ni kweli tuna mkutano mkuu utakaofanyika mkoani Dodoma, ila tarehe bado hatuja confirm (hatujathibitisha) mapendekezo ya awali ni kati ya Septemba 10 au 24 na kwa sababu hatujathibitisha tarehe bado hatujawaarifu wajumbe,” alisema Selasini.
Alipoulizwa kuhusu agenda za mkutano mkuu huo, Selasini alisema unakwenda kujadili mashtaka yanayomkabili Mbatia, ambayo kwa katiba ya chama, Halmashauri Kuu iliyoketi Mei 21 haikuwa na mamlaka ya kusikiliza na kuamua.
“Kama unakumbuka kile kikao halali kabisa cha Halmashauri Kuu kilimzuia Mbatia na Martha kufanya shughuli zozote za chama hadi atakapojitetea mbele ya mkutano mkuu na wajumbe kutoa uamuzi wao,” alisema Selasini.
Kinachoweza kumtokea Mbatia na wanaomuunga mkono, kinaweza kufanana na kile kilichotokea Machi 2019 kwa aliyekuwa mwanasiasa mkongwe na katibu mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad kutimkia ACT-Wazalendo.
Maalim Seif na wale wanaomuunga mkono, walifikia uamuzi huo baada ya Mahakama Kuu kumhalalisha Profesa Ibrahim Lipumba kuwa Mwenyekiti halali wa CUF na kuhitimisha mgogoro uliodumu kwa zaidi ya miaka miwili tangu Profesa Lipumba abatilishe uamuzi wake wa kujivua uenyekiti wa CUF, Agosti mwaka 2015 na kurudi madarakani mwaka 2016. Maalim Seif, aliyefariki dunia Februari 17 mwaka jana akiwa mwenyekiti wa ACT-Wazalendo na Makamu wa kwanza wa Rais Zanzibar, alihitimisha safari ya uanachama na uongozi ndani ya CUF alikohudumu kwa zaidi ya miaka 20 akitokea Chama cha Mapinduzi (CCM).
Mbatia ajiandaa kujiunga Chadema?
Wakati NCCR-Mageuzi upande unaoungwa mkono na ofisi ya Msajili ukiitisha mkutano huo, kumekuwa na taarifa zinazosambaa katika mitandao ya kijamii kuwa Mbatia anajiandaa kujiunga na Chadema.
Katika mitandao hiyo ya kijamii, yakiwamo makundi ya Whatsapp yenye uhusiano na Chadema, kumekuwa na wanajukwaa wanaoandika maneno kama “Karibu Chadema Mbatia”, huku wengine wakidai amekata shauri kujiunga Chadema.
Mbatia mwenyewe alipotafutwa jana kuzungumzia hicho kinachoendelea katika mitandao ya kijamii, hakukubali wala kukataa zaidi ya kujibu kwa kifupi tu kuwa “Hilo nitalitolea ufafanuzi baadaye”.
Hata hivyo, alipotakiwa kuzungumzia mkutano mkuu ulioitishwa na kina Selasini, Mbatia alisema kama ni msimamo wa chama, basi utatolewa na Mkuu wa Idara ya Uenezi na Uhusiano wa Umma wa NCCR-Mageuzi, Edward Simbeye.
Alipotafutwa Simbeye, aliwataka wanachama wa chama hicho nchi nzima kuwa watulivu, akisema hakuna kitu kinaitwa mkutano mkuu utakaofanyika wiki ijayo, akisisitiza kuwa hicho kilichotangazwa na Selasini na kundi lake ni porojo tu.
“Msimamo wa nini chama kitafanya tutautoa Jumatatu wiki ijayo na tutasema nini tutafanya kurudisha chama kwenye msitari,” alisema.
Simbeye alifafanua kuwa kikao kilichoitwa ni cha Halmashauri Kuu ya NCCR-Mageuzi, kilichokutana Mei 21, 2022 na kutoa maamuzi ya kumsimamisha Mbatia na Martha wakisubiri hatua zaidi za mkutano mkuu, kilikuwa haramu.
“Kikao chetu cha Halmashauri kuu kilichofanyika Agosti 13 (2022) kilielekeza tu tuendelee na maandalizi ya chaguzi za ndani na wala hatuna schedule (ratiba) ya mkutano mkuu. Hicho wanachokisema akina Selasini ni porojo,” alisisitiza.
“Tuna taarifa jana akina Selasini waliitisha kikao Kibamba na kukusanya vijana wakiwavalisha T-shirt (fulana) za NCCR-Mageuzi ili wakiulizwa waseme ni wajumbe wa mkutano mkuu toka mikoani. Huu ni uhuni,” alisema Simbeye.