NILIKUWA pale Luanda, Angola na Namungo iliyokwenda kucheza na Clube Desportivo 1 de Agosto mwaka jana. Lakini wageni hawakugusa mpira hata wa mazoezi kutokana na vihoja kutawala nje ya Uwanja.
Simba msimu huu imepangwa kucheza na klabu hiyo katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika, kati ya Septemba 7-9, mwaka huu jijini Luanda. Ngoja nikupe stori sasa.
Historia ya karibuni ya klabu za Tanzania dhidi ya Clube Desportivo 1 de Agosto, ni tafrani za mchezo wa kwanza wa Kombe la Shirikisho Afrika uliopangwa kuchezwa Februari 14, 2021.
Mchezo huo wa kufuzu hatua ya makundi msimu wa 2020-21, ulipangwa kuchezwa kwenye Uwanja wa Novembro 11 uliopo Talatona, pembeni kidogo ya Luanda, Angola.
Kabla ya Namungo kuondoka Dar es Salaam, mchezaji wao mmoja akiwa kwenye ngazi za kupanda kwenye ndege aliwaambia viongozi kwamba hataki kuendelea na safari kwa madai kwamba roho yake inasita. Wakamtema akarudi zake nje, sisi tukaondoka.
NAMUNGO HAIKUGUSA MPIRA ANGOLA
Tukatua Luanda sasa. Chini ya Kocha Hemed Morocco wakati ule, Namungo FC ilifika kwa lengo la kufanya mazoezi ya siku mbili kisha kucheza dhidi ya Clube Desportivo 1 de Agosto.
Msafara ulipowasili Uwanja wa Ndege wa Luanda, usiku wa manane, ulikutana na kigingi cha kipimo Uviko-19. Watu wanne kwa maana ya kiongozi mmoja na wachezaji watatu walikutwa na vimelea vya ugonjwa huo.
Wataalam wa afya waliovalia mavazi ya kijeshi ndiyo waliohusika na upimaji wa Uviko-19, na kwa mujibu wa kanuni za afya za Angola kwa wakati ule, wanne hao wakatakiwa kutengwa.
Pia ikatoka amri ya msafara mzima kwenda karantini, umbali wa kilomita zaidi ya 200 yaani umbali wa kutoka Dar es Salaam mpaka Morogoro. Msafara ulitumia saa zaidi ya tatu kufika huko.
Kumbuka msafara kabla ya haujaondoka Dar es Salaam wakati huo, watu wote walipimwa Uviko-19 na kuonekana hawana maambukizi.
Kasheshe ni kwamba hakuna mtu aliyekubali kushuka katika basi kuingia katika vyumba vilivyotengwa kama karantini ambako ingebidi wote wakae kwa siku saba.
NAMUNGO YARUDI TANZANIA, YAFUZU
Baada ya majadiliano ya saa 24, hatimaye msafara wa Namungo ukarejea Tanzania Februari 15, 2021 na siku chache baadaye CAF ikatoa taarifa nzima kuhusu tukio hilo.
CAF ikaamuru mechi zote mbili sasa zichezwe Tanzania ambapo katika mchezo wa kwanza, Namungo Februari 21, ilishinda mabao 6-2 na katika marudiano Februari 25 ikafungwa mabao 3-1, hivyo wakafuzu kwa mabao 7-5. Namungo ikafuzu hatua ya makundi. Huko kwenye makundi walipigwa mechi zote sita nje ndani.
SIMBA IJIANDAE
Kwa hali niliyoiona Luanda wakati ule ni muhimu Simba itazame haraka ratiba za ndege lakini kuwa kwenye mazingira salama zaidi ni bora kukodi ya kwao.
Bado kanuni za afya zinaweza kuigharimu Simba ukizingatia tahadhari ya Uviko-19 ikiwa bado ipo katika nchi nyingi za Afrika, hapo ndipo mahali penye umakini zaidi.
Timu ya Afya ya Simba inatakiwa kujiamini na kushirikiana kwa karibu na watu wa afya watakaokuwa wakipima kwenye uwanja wa ndege mara tu baada ya kuwasili Angola na hapa ni muhimu sana kutanguliza watu mapema na kuweka mazingira mazuri na Ubalozi wetu kwa lolote litakalotokea.
Timu nyingi za Afrika Kaskazini hufanya hivi zinapofika Tanzania na uhakika wa daktari katika kusimamia zoezi la upimaji hupunguza hujuma za wapinzani. Ingawa wenzetu wameweka mbele zaidi masilahi ya timu zao.
Clube Desportivo 1 de Agosto ni timu iliyoanzishwa Agosti Mosi, mwaka 1977 ikiwa sehemu ya Jeshi la Angola na inadhaminiwa na jeshi hilo. Inaendeshwa kiraia lakini kuna mikono ya jeshi katika utawala.
Labda wabadilike safari hii kwa kuhofia jina la Simba. Lakini umbali wa kutoka Luanda mpaka kutakapochezwa mechi ni mbali. Na hii hufanyika kimkakati kumdhohofisha mgeni.
VIFO VYA WATU WATANO UWANJANI
Simba itacheza na Clube Desportivo 1 de Agosto kwenye Uwanja wa Taifa wa Novembro 11, uliopo eneo la Talatona umbali wa Kilomita 17 kutoka Luanda. Jina la Uwanja huu limetokana na siku ya Uhuru wa Angola ambayo ni 11 Novemba, 1975.
Uwanja huu unaingiza watu 48,000 walioketi na ulitumika katika fainali za Kombe la Afrika mwaka 2010, mechi ya fainali ilichezwa hapo.
Kama ilivyo kwa Uwanja wa Benjamin Mkapa kutumiwa na klabu kubwa nchini, Uwanja wa Novembro 11, licha ya Clube Desportivo 1 de Agosto pia unatumiwa na klabu za Petro de Luanda na Benfica zinazoshiriki Ligi Kuu ya Angola.
Jumamosi ya Septemba 15, 2018, watu watano waliripotiwa kufariki baada ya umati wa mashabiki kukanyagana wakati wakitoka uwanjani baada ya mchezo kati ya Clube Desportivo 1 de Agosto na TP Mazembe.
Huo ulikuwa mchezo wa robo fainali wa Ligi ya Mabingwa Afrika ambapo Clube Desportivo 1 de Agosto ilitoka suluhu na TP Mazembe na hata katika mchezo wa marudiano Septemba 21, timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1 nchini DRC na Clube Desportivo 1 de Agosto wakasonga mbele.
Wizara ya Michezo na Vijana Angola iliomba radhi kwa vifo hivyo, ikatuma salamu za pole kwa familia za marehemu na kuahidi kufanya uchunguzi, huku klabu ikigharamia gharama za mazishi kwa wafiwa.