Onyango arejea kibabe, apewa gari





BEKI wa Simba, Mkenya Joash Onyango ambaye alikuwa analazimisha kuondoka kikosini, jana alikuwa miongoni mwa mastaa waliosafiri na timu kwenda Mbeya.

Awali, Onyango alipeleka barua katika Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kuomba kusitishiwa mkataba wake wa miaka miwili na kati ya sababu alizoeleza ni kushindwa kutimiziwa mahitaji yake pamoja na kupoteza nafasi yake kwenye kikosi cha kwanza mbele ya kocha aliyeondoka Zoran Maki. Onyango inadaiwa alikuwa akishinikiza kuondoka ili ajiunge na Singida Big Stars lakini Simba wakashtukia mchezo wakamuita mezani.

Beki huyo kwenye maboresho yake ya mkataba mpya alihitaji kupewa gari, Sh70 milioni na kuboreshewa samani za ndani kwake. Habari za uhakika ni kwamba hayo yote yametekelezwa kwa asilimia kubwa na ameridhia kuendelea kupiga mzigo sasa akiangukia mikononi mwa Kocha Juma Mgunda.

Habari za uhakika zinasema kwamba Simba walimuita mezani baada ya kushtukia kwamba analazimisha kuondoka kimyakimya kwa mlango wa Singida lakini ataibukia Jangwani ambao walipanga kuimarisha safu yao ya ulinzi.


Akizungumza na Mwanaspoti, Onyango licha ya kutotaka kuingia kiundani alisema kwa kifupi; “Naungana na timu leo (jana) kwaajili ya mchezo wetu wa Jumatano na Tanzania Prisons, tumeshamalizana.”

Tangu beki Mohamed Ouattara atue Simba, Onyango hajapata nafasi ya kucheza mechi yoyote kwani hakuwa na wakati mzuri na Zoran baada ya kuanza kudai masilahi yake ni kujiondoa kambini.

Kabla ya ujio wa beki huyo, Simba ilikuwa na Pascal Wawa ambaye ameachwa baada ya mkataba wake kuisha, Henock Inonga na Onyango ambao walikuwa wanapeana nafasi ya kucheza huku Inonga na Onyango wakipewa nafasi kubwa ya kucheza kikosi cha kwanza.


Wawili hao wamecheza pamoja kwenye mechi 10 kati ya 18 za Ligi Kuu tangu Inonga ajiunge na Simba katika dirisha dogo huku wakiruhusu mabao 4 kati ya sita waliyofungwa Simba kipindi hicho.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad