IMEISHA hiyo. ndivyo unavyoweza kusema baada ya beki wa kati wa Simba, Joash Onyango kumalizana na mabosi wake Msimbazi, baada ya awali kutaka kusitisha mkataba wake kutokana na kuhitaji kutimiziwa maslahi kwenye kandarasi yake mpya, hii ni kufuatia kufanya kikao kizito kuwekana sawa.
Habari kutoka ndani ya Simba zinasema juzi Jumanne, Onyango alikutana na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa klabu hiyo, Salim Abdallah ‘Try Again’ na Mkenya huyo alizungumza changamoto zilizokuwa zinamkabili hadi kushindwa kwenda Sudan na kutoa msimamo wa kutaka aachwe na Wekundu hao.
Baada ya kuzungumza yote hayo mwisho alieleza vitu ambavyo anataka kutimiziwa katika mkataba wake mpya ili arudi mchezoni pamoja na kusahau yale mengine yote aliyokuwa anapitia wakati huu.
Kwe-nye kikao hicho, Try Again alikubaliana na Onyango na alikubali kujiunga na kikosi mara baada ya kurejea nchini Septemba Mosi kikitokea Sudan kilipokwenda kucheza mechi mbili za kirafiki.
Kutokana na makubaliano hayo ya Simba na Onyango maana yake dili la kwenda kujiunga na Singida Big Stars kama ilivyokuwa awali litakuwa limekufa na atasalia kwenye kikosi hicho kuendelea kuutumikia mkataba wake wa miaka miwili aliosaini kabla ya msimu huu kuanza.
Mchezaji huyo ataungana na wachezaji wenzake kwenye mazoezi mara baada ya kikosi hicho kurejea nchini ili kufanya maandalizi ya mchezo wa kimataifa wa kirafiki dhidi ya Arta Solar 7 Septemba 3 na mashindano.
Onyango aligoma kwenda Sudan kutokana na kushindwa kutimiziwa baadhi ya maslahi pamoja na suala la kuwekwa benchi na yote hayo yamezungumzwa na kufika mwisho na sasa kazi imebaki kwake.
Mwanaspoti lililpomtafuta Onyango kuzungumza naye alisema: “Masuala yote ya mkataba uongozi wangu ndio una nafasi ya kuzungumza zaidi kwani mimi kazi yangu ni kucheza.”
Kwa upande wake, Try Again alisema Simba haiwezi kumuachia Onyango kutokana na mchango wake katika timu kwa kuwa amekuwa akifanya kazi nzuri kwa kushirikiana na wachezaji wenzake tangu alipofika na changamoto zilizotokea ni sehemu ya maisha kwenye soka.
“Onyango ataendelea kubaki Simba na atakuwa sehemu ya kikosi baada ya kurejea kutoka Sudan. Nilikutana naye juzi na kuongea tulimaliza mazungumzo yetu akiwa hana shida yoyote ile,” alisema. “Hakuna shida yoyote na Onyango, ameniahidi anarudi kazini akiwa na nguvu zote kuipigania Simba. Yote na yaliyopita ameshayasahau.” Simba baada ya mechi jana ilitarajiwa kuanza safari kurejea nchini na inatarajiwa kutua saa 7 mchana.