Dar es Salaam. Jeshi la Polisi limewataka wananchi walioibiwa mali zao kujitokeza katika vituo vya polisi ili kuzitambua.
Wito huo imetolewa ikiwa ni siku chache tangu kuibuka kwa matukio ya uvamizi wa kutumia silaha za jadi, kisha kujeruhi na kupora vitu mbalimbali nyakati za usiku yanayokwenda sambamba na yanayofanywa na Panyarodi.
Akizungumza na waandishi wa habari juzi katika Kituo Kikuu cha Polisi Mkoa wa Kinondoni, Kamishna wa Operesheni na Mafunzo nchini, Awadhi Haji aliwataka wananchi kujitokeza kwenye vituo vya Buguruni, Stakishari, Chang’ombe, Mbagala, Kawe na Kimara kutambua mali zao.
“Jeshi la Polisi linaendelea kutoa wito kwa wananchi wote na wadau mbalimbali kuendelea kutoa ushirikiano kwa kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu, ili hatua stahiki zichukuliwe kabla ya vitendo hivyo havijatokea,”alisema Kamishna Haji.
Akizungumzia Operesheni iliyofanyika Septemba alisema watuhumiwa 167 wa vitendo vya kihalifu ikiwemo kuvunja usiku, kujeruhi kwa kutumia silaha za jadi kama vile visu, mapanga na nondo walikamatwa.
“Watuhumiwa hao wamegawanyika katika makundi mawili, kuna kundi la wanaoshiriki moja kwa moja kuvunja na kufanya uporaji na linalopokea na kununua mali za wizi” alisema.
Alibainisha kuwa katika operesheni hiyo walifanikiwa kukamata mali zilizoibiwa katika maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam ambazo ni televisheni 23, redio mbili, kompyuta mbili na spika mbili.
“Miongoni mwa watuhumiwa waliokamatwa walikutwa na mapanga 19, vifaa vya kuvunjia, mikasi minne, nondo saba na jeki mbili.
“Pia tumefanikiwa kukamata magari matatu, pikipiki tano walizokuwa wakutumia wahalifu hao kubeba zana za kufanyia uhalifu pamoja na kusafirishia mali baada ya kufanya uhalifu,”alisema.
Kamishna Haji alisema watuhumiwa hao pia walikamatwa na dawa za kulevya aina ya Heroine gramu 35, bangi kilogramu 63 na mirungi kilogramu tisa.
“Operesheni hii ni endelevu na itafanyika nchi nzima ili kukabiliana na vitendo vya kihalifu kama vilivyokuwa vinafanyika Dar es Salaam, ambavyo tayari vimedhibitiwa kwa kiwango kikubwa na sasa hali ni shwari.
“Jeshi la polisi linawahimiza wananchi kuanzishwa na kuimarisha vikundi vya ulinzi shirikishi, ili kuimarisha ulinzi kwenye maeneo yao,”alisema.
Hivi karibuni kumeibuka wimbi la vitendo vya kihalifu vya unyang’anyi wa kutumia silaha vinavyofanywa na kundi la wahalifu wanokadiriwa kuwa na miaka 14 hadi 30.
Miongoni mwa matukio hayo ni pamoja na tukio la mauaji ya mwanafunzi wa mwaka wa pili wa Shule ya Uandishi wa Habari Dar es Salaam (SJMC) Maria Basso, baada ya vijana waliokuwa na silaha za jadi kuvamia nyumbani kwao Kawe Mzimuni usiku wa kuamkia Septemba 14.
Tukio lingine kama hilo lilitokea siku hivyo hiyo mtaa wa Dovya Chamanzi, wilayani Temeke ambapo vijana wakiwa na mapanga, nondo na marungu walivamia, kujeruhi na kuiba vitu mabalimbali vikiwemo simu, runinga na fedha.