Polisi Wengine Arusha Wadaiwa Kupora Mil 6/-



POLISI wanne mkoani Arusha wanadaiwa kumpora mfanyabiashara wa mazao Sh milioni sita.

Hali hiyo imejitokeza zikiwa zimepita siku kadhaa baada ya polisi wengine watatu kudaiwa kumpora mfanyabiashara mwingine wa mazao Sh milioni tatu, Agosti 25 mwaka huu.

Inadaiwa kuwa Septemba 6 mwaka huu saa 1.30 usiku, askari wanne akiwemo Mkuu wa Kituo cha Polisi Ngaramtoni kilichopo wilayani Arumeru mkoani Arusha (majina tunahifadhi kwa sasa), walikamata fuso la mfanyabiashara huyo lililokuwa limetoka Oldonyosambu likiwa limebeba mahindi.

Vyanzo vya habari kutoka Kituo cha Polisi Ngaramtoni vilidai kuwa, askari hao walidai mfanyabiashara huyo alikwepa ushuru na walitaka awape rushwa ya Sh milioni 30 wamwachie.


Ilidaiwa kuwa, mfanyabiashara huyo aligoma kutoa rushwa, polisi walilipekua gari hilo na mabegi yake na walikuta Sh milioni sita wakazichukua.

Vyanzo vilidai kuwa, Septemba 8 mwaka huu mmiliki wa fuso hilo na mfanyabiashara huyo (majina tunahifadhi kwa sasa) walikwenda kwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Justine Masejo kumweleza mkasa huo.

Ilidaiwa kuwa, walalamikaji waliulizwa kama wanaweza kuwatambua watuhumiwa na wakasema wangeweza hivyo polisi waliokuwa zamu Septemba 6 mwaka huu waliitwa ofisini kwa Kamanda Masejo.


Chanzo kilidai kuwa walalamikaji waliwatambua watuhumiwa na wafanyabiashara hao walimweleza Kamanda Masejo kuwa wao walihitaji fedha zao.

Inadaiwa kuwa, Kamanda Masejo aliamuru polisi hao warudishe fedha walizodaiwa kuzipora, nao waliomba muda wa saa moja na baada ya saa mbili walirudisha Sh milioni sita walizodaiwa kuzipora.

Kamanda Masejo hajakanusha au kuthibitisha kutokea kwa jambo hilo na alisema uchunguzi wa matukio ya uporaji unaodaiwa kufanywa na polisi Arusha ukikamilika atatoa taarifa.

Agosti 25 mwaka huu polisi watatu akiwemo Mkuu wa Kituo cha Polisi Engutoto jijini Arusha, Mahamud Jakaya, walidaiwa kumpora mfanyabiashara za mazao, Ramadhani Hamisi kutoka Dodoma Sh milioni tatu.

Ilidaiwa kuwa uporaji huo ulifanywa saa 4 usiku katika eneo la Kwa Mrombo jijini Arusha.

Chanzo kilitaja polisi wengine waliodaiwa kuhusika kwenye uporaji huo kuwa ni Ramadhani Mcheka na Mkaguzi Msaidizi aliyetambuliwa kwa jina moja Machanganya.

Ilidaiwa kuwa mfanyabiashara aliwatambua baada ya kufanyika gwaride la utambuzi na askari hao walirudisha Sh milioni 2.5

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad