Dar es Salaam. Mbunge wa Ubungo (CCM), Profesa Kitila Mkumbo amesema Katiba mpya ni muhimu kwa sababu itaongeza ushiriki wa wananchi katika demokrasia.
Profesa Kitila ameyasema hayo jana Alhamisi Septemba 16, 2022 jijini Dar es Salaam wakati wa kongamano la maadhimisho ya siku ya kimataifa ya demokrasia ambayo iliwakutanisha wadau mbalimbali kujadili miaka 30 ya demokrasia ya Tanzania.
Amesisitiza umuhimu wa kuandikwa kwa Katiba mpya ambayo itawashirikisha wananchi na itawapa fursa ya kukuza demokrasia yao.
“Ni vizuri iandikwe katiba ambayo itaongeza ushiriki wa wananchi katika demokrasia. Katiba ikiendelea namna hii, mtaendelea kulia kila mwaka,” alisema Profesa Kitila.
Mbunge huyo alisema ili wananchi washiriki vizuri katika demokrasia, lazima miiba iliyopo kwenye demokrasia hapa nchini iondolewe. Aliwataka wananchi kupigania demokrasia kuanzia ndani ya vyama vyao.
“Hakuna namna nchi inaweza kupata maendeleo bila kukumbatia demokrasia. Tupiganie sana demokrasia yetu. Haki duniani huwa haiombwi, upendeleo ndiyo unaombwa.”
“Demokrasia haiwezi kushamiri kama ndani ya vyama hakuna demokrasia. Tuhakikishe tunaimarisha demokrasia ndani ya vyama vyetu kwanza kabla ya kutoka nje,” alisisitiza Profesa Kitila.
Profesa Kitila Mkumbo alisema Tanzania inakabiliwa na udumavu wa vyama vya siasa, jambo ambalo limekuwa likiifanya CCM iendelee kushinda chaguzi uchaguzi.
Mwanazuoni huyo alisema uchaguzi wa Tanzania unatabirika tofauti na Kenya ambako huwezi kumjua mshindi.