Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais mstaafu, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Malecela, amewahi kujiita “Tingatinga”, kwamba yeye huchonga barabara.
Kabla ya Malecela kujiita Tingatinga, tayari Waziri Mkuu mstaafu Kenya, Raila Odinga, alishapewa jina hilo. Jina ambalo linajenga tafsiri pana kwa Raila katika maisha yake ya kisiasa.
Mwaka 1994, Raila alipojiunga na chama cha Maendeleo ya Kitaifa (National Development Party ‘NDP’), kutokea Ford Kenya, ilizaliwa kauli mbiu ya Tinga, kifupi cha Tingatinga. Awali Tinga ilikuwa kauli mbiu ya chama, lakini ilijitengeneza zaidi kama jina la utani la Raila.
Tingatinga huchonga barabara lakini ikishawekwa lami, huwa haliruhusiwi kupita juu yake, maana litaharibu. Kama ilivyo sifa ya jina Tinga, ndivyo na Raila. Amechonga barabara ya siasa Kenya. Amekuwa chemchemi ya demokrasia na ujio wa mfumo wa vyama vingi vya siasa.
Ndani ya miaka 25, amegombea urais mara tano na hakufanikiwa. Mwaka 1997 lilikuwa jaribio lake la kwanza na 2022 ni la tano. Ameanguka lakini haina maana katika hiyo miongo miwili na nusu Raila amefeli, la! Ameshinda kila kitu isipokuwa urais wa Kenya.
Amechochea mageuzi
Kwa miaka 40 iliyotimia, Raila amekuwa mwanasiasa aliyefanikisha mengi au aliyechochea mageuzi ya kidemokrasia ambayo Kenya wapo nayo leo. Kuanzia mfumo wa vyama vingi vya siasa mpaka kupatikana kwa Katiba ambayo imeweka misingi kwa nchi hiyo kufanya uchaguzi huru, haki na wenye kuaminika.
Mwandishi gwiji wa Kenya na Afrika, Profesa Ngugi wa Thiong’o, amewahi kuandika kuhusu Raila jinsi alivyo jasiri, aliyevumilia mateso jela kwa ajili ya kupigania mfumo wa demokrasia ya vyama vingi.
Ngugi aliandika kuhusu mateso ambayo Raila aliyapata akiwa gerezani. Alimpoteza mama yake mzazi akiwa nyuma ya nondo na wala hakutetereka. Vilevile vipigo vilivyokaribia kumfanya awe mlemavu, navyo havikumfanya asalimu amri.
Mtaalamu huyo wa fasihi andishi duniani, aliandika kuwa Raila alipotoka jela hakwenda nyumbani kwake, alimfuata na kumshawishi kuungana naye ili kuendeleza harakati za kupigania mfumo wa vyama vingi vya siasa.
Ngugi akasema, ni harakati hizo ndizo zilichochea mabadiliko na Kenya kuupokea mfumo wa vingi vya siasa. Madhumuni ya Ngugi yalikuwa kutaka watu wafahamu kwamba Raila si mtu mwoga. Ni mpambanaji.
Mantiki ninayotaka ipenye kwenye kila kichwa ni kwamba Raila ni mshindi. Alipigania mfumo wa vyama vingi vya siasa kwa jasho, machozi na damu. Alifungwa miaka minane jela, aliwekwa kizuizini nyumbani kwake na mara kadhaa mahabusu. Hata hivyo, hakurudi nyuma hadi ushindi ulipopatikana.
Kenya ilipofanya Uchaguzi Mkuu wa kwanza uliohusisha vyama vingi vya siasa mwaka 1992, Raila aliuendea uchaguzi na tabasamu. Alikuwa mshindi. Alifanikisha malengo. Alichonga barabara ya demokrasia ambayo inavutia Afrika na duniani.
Alivyonusurika kuuawa
Oktoba 1991, Raila alikimbia nchi. Alikwenda mafichoni Norway, baada ya kunusurika kuuawa mara kadhaa. Raila alisema, Serikali ya Kenya chini ya Daniel Moi, ilikusudia kumuua ili kumnyamazisha aliendelee kukosoa. Hapa ina maana kuwa hata uhai wa Raila leo ni ushindi. Alishinda vita ya kupigania uhai wake.
Uchaguzi Mkuu Kenya 1992, Raila hakugombea urais. Alirejea Kenya kutokea uhamishoni Norway na kuungana na baba yake, Jaramog Odinga, aliyetoka wa tatu nyuma ya Moi na Kenneth Matiba. Raila aligombea ubunge jimbo la Lang’ata na kushinda.
Raila aliliongoza jimbo la Lang’ata kwa miaka 20. Hakuna wakati wowote Raila aliwahi kushindwa uchaguzi wa ubunge. Hivyo, katika mapambano jimboni na siasa za ndani ya Bunge la Kenya, Raila ni mshindi.
Baada ya Uchaguzi Mkuu Kenya 1997, Raila baada ya kushindwa kiti cha urais, alifanya mapatano na Moi. Kisha chama chake, NDP kikaungana na chama tawala cha Kenya African National Union (Kanu). Baada ya kuungana na Moi, alipanda ngazi mpaka kuwa Katibu Mkuu wa Kanu.
Raila kuwa Katibu Mkuu wa Kanu ulikuwa ushindi mwingine. Ilikuwa kudhihirisha nguvu zake kiasi cha kumlazimu Rais Moi kufanya naye mazungumzo na hata kumpokea kuwa Katibu Mkuu wa Kanu, kisha akamfanya kuwa Waziri wa Nishati.
Kwa wananchi wa Nyanza, eneo analotokea Raila, kwa miaka mingi walikuwa hawapokei maendeleo na kukosa huduma za msingi kutoka serikalini kutokana na uhusika wa siasa za upinzani wa Jaramog (baba wa Raila) na Raila mwenyewe.
Nyanza iliwakumbatia Jaramog na Raila, kwa kitendo hicho jumlisha na maisha ya siasa za ukabila Kenya, Moi akaamua kulitenga eneo hilo. Baada ya Raila kuungana na Moi, Nyanza ilianza kupata maendeo na huduma nyingi serikalini. Hili pia la kufanikisha maendeleo Nyanza, Raila alishinda.
Moi alivyomuangusha
Uchaguzi Mkuu 2002, wengi walidhani Moi angempigia chapuo Raila kuwa mrithi wake. Kinyume chake alichagua kusimama na Uhuru Kenyatta, mtoto wa mtangulizi wake.
Uamuzi wa Moi ulimuudhi Raila, aliyeungana na wanasiasa wengine wenye majina makubwa Kanu, kumsusia chama Moi na Uhuru wake, wakaenda kusimamisha ushirika wa kisiasa wa National Rainbow Coalition (Narc).
Narc walimteua Mwai Kibaki kuwa mgombea urais. Raila aliibeba tiketi ya Kibaki na kuzunguka Kenya nzima akiomba achaguliwe dhidi ya Uhuru. Raila alifika Mlima Kenya, nyumbani kwa Uhuru na Kibaki. Akawaeleza kwa nini Kibaki na sio Uhuru.
Wananchi waliitikia. Kibaki alishinda. Sio hivyo tu, Kanu iliondoka kwenye uongozi wa siasa za nchi, kikageuka chama cha upinzani. Kitendo cha kuiangusha Kanu na Moi, kisha kumwingiza madarakani Kibaki kilitafsiri ushindi mkubwa kwa Raila. Uchaguzi Mkuu 2002, Raila alishinda.
Makubaliano yaliyounda Narc mwaka 2002, yalijengwa sharti kuwa kama Kibaki angeshinda urais, angemteua Raila kuwa Waziri Mkuu. Kibaki hakutekeleza hilo, alimfanya Raila kuwa Waziri wa Barabara, Ujenzi wa Umma na Nyumba.
Raila aliihudumia wizara hiyo kwa miaka miwili na miezi 10, baada ya hapo alisimama kama mpinzani halisi. Chanzo kilikuwa Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2005. Kibaki na viongozi wengi serikalini walitaka mabadiliko ya Katiba.
Upande wa Raila, aliona mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2005 hayakuwa na afya njema kwa Kenya. Ndani ya Bunge la Katiba lilizaliwa vuguvugu lililoitwa Orange Democratic Movement (ODM). Raila alikuwa sehemu ya ODM na kupinga mabadiliko ya Katiba.
ODM walizidiwa nguvu na wabunge waliotaka mabadiliko ya Katiba. Rasimu inayopendekezwa ikapita kwa ajili ya kupigiwa kura na wananchi. Kibaki na Serikali walifanya kampeni ya “Ndio”, Raila na ODM walisema “Hapana”.
Wananchi walipopiga kura Novemba 21, 2005, asilimia 58.35 walipiga kura ya Hapana. Asilimia 41.65 walisema Ndio. Mabadiliko ya Katiba 2005 yakakwama. Hapa Raila alishinda. Tena ushindi mkubwa kabisa.
Baada ya kufeli kwa mabadiliko ya Katiba 2005, ODM ilisajiliwa kama chama cha siasa. Raila akawa kiongozi. Na kwa kuwa alishatofautiana waziwazi na bosi wake, aliondoka Baraza la Mawaziri. Ikawa zamu ya kuongoza upinzani.
Machafuko ya uchaguzi
Ukawadia Uchaguzi Mkuu 2007. Mchuano mkali ukawa baina ya Kibaki na Raila. Matokeo yalipotoka yalisababisha mtafaruku na hata vifo. Kila upande ulitamba kushinda uchaguzi.
Kutuliza vurugu ilibidi Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa waingilie kati. Kikao cha usuluhishi kilichoongozwa na aliyekuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika, Jakaya Kikwete, kiliwapatanisha Kibaki na Raila, kwamba mmoja aendelee kuwa Rais, mwenzake awe Waziri Mkuu.
Kwa hakika, ilikuwa dhambi ya damu kumwagika ambayo chanzo chake alikuwa aliyekuwa Mwenyekiti Sam Kivuitu na wanasiasa wa pande zote. Kila mmoja kung’ang’ania ushindi, mwisho damu za watu wasio na hatia zilimwagika.
Ukiondoa dhambi ya damu kumwagika, Raila alishinda mapambano ya mwaka 2007-2008, maana alifanikiwa kiwa Waziri Mkuu, cheo ambacho awali Kibaki alimnyima mwaka 2002.
Machafuko ya mwaka 2007-2008, yalichochea mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2010. Raila ni mshindi katika mafanikio ya Kenya kupata Katiba mpya ambayo imeweza kuimarisha taasisi na kuzipa uhuru kuliko wakati wowote katika historia ya nchi hiyo, na vilevile kuliko mataifa mengi Afrika na duniani.
Katiba ya Kenya ya mwaka 2010 ni sababu Uchaguzi Mkuu 2017, matokeo yaliyompa ushindi Rais Uhuru Kenyatta, kubatilishwa. Aliyepeleka mashtaka mahakamani kupinga matokeo alikuwa Raila.
Kwa mara nyingine, Raila aliibuka mshindi mwaka 2017 kwa Kenya kuweka historia ya Bara la Afrika zima kwa ushindi wa Rais kutenguliwa mahakamani.
Raila alishinda kila kitu kasoro urais. Kila jaribio la urais lilifeli. Hata mpango wa kumpindua Rais Moi mwaka 1982 ulifeli. Raila aliwahi kukiri kuwa sehemu ya jaribio hilo la mapinduzi ya Moi.
Jina jingine Raila ni Baba. Wanamwita Baba wa Siasa Kenya. Ni baba ambaye amelea watu wengi na kuwafundisha siasa, ila hajaweza kushika nafasi ya juu ya kisiasa. Ofisi namba moja Kenya. Rais wa Jamhuri.
Swali kubwa linalotawala vichwani mwa Wakenya, nini hatima ya Odinga baada ya kushindwa urais kwa mara ya tano huku akiwa anaungwa mkono na Rais Uhuru Kenyatta?
Kauli ya Ruto
Juzi mara baada ya Mahakama ya Juu ya Kenya, kuthibitisha ushindi wa Ruto mwanasiasa huyo ameahidi kufanya kazi na Raila kwa nafasi yake ya upinzani si vinginevyo.
“Tunataka siasa za Kenya kwa siku zijazo ziwe nzuri na kila mwanasiasa awajibishwe kwa kile alichokisema, kila kiongozi amaanishe kile alichokisema na tunataka mfumo wa haki za jinai usitumike kwa sababu za kisiasa, hatutaki utumike kwa watu watakaokuwa na mawazo tofauti na sisi”alisema
“Washindani wetu hawana cha kuhofia kama baadhi ya wafuasi wetu walivyokuwa wakihofu, alisema”
Raila akubali yaishe
Mara baada ya hukumu hiyo, Odinga alisema anaheshimu uamuzi huo lakini hajakubaliana nao.
“Tunaheshimu uamuzi wa mahakama ingawa hatukubaliani nao na wataangalia namna nyingine ya kuendeleza siasa za kudumisha demokrasia, uwazi na uwajibikaji,” alisema
Rais Kenyatta
Rais Uhuru Kenyatta, juzi mara baada ya hukumu hiyo alisema maandalizi ya kukabidhi madaraka yanaendelea vizuri na akawataka Wakenya kuendelea kuwa wamoja.
“Ninataka kuwatakia kila la kheri wote ambao wameshinda wanapoenda kuongoza nchi yetu katika siku zijazo. Ninawashukuru wote kwa fursa mlionipa ya kuwahudumia,” alisema Kenyatta.
“Taratibu zote za muhimu za kufanyika mchakato huu (kukabidhi madaraka) tayari zimefanyika na ninaamini mambo yatakwenda sawa kama yalivyopangwa,” alisema.
Alisema yeye ni muumini wa mifumo ya utawala, kuheshimu sheria na Katiba hivyo baada ya Mahakama ya Juu kuidhinisha ushindi wa Ruto kinachofanyika sasa ni kutekeleza kile kilichoamriwa.