Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amewapongeza wananchi wa Kenya kwa kuonyesha ukomavu wa demokrasia huku akisema wametoa zawadi pekee ya amani wakati wa uchaguzi kwa nchi nyingine za Afrika Mashariki.
Rais Samia ameeleza hayo leo Septemba 13, 2022 jijini Nairobi wakati wa sherehe za kuapishwa kwa William Ruto kuwa Rais, ambaye alishinda uchaguzi mkuu uliofanyika Agosti 9 na kutangazwa na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).
Rais Samia amesema wananchi wa Kenya wameonyesha ukomavu wa demokrasia Afrika Mashariki na kusisitiza kwamba sasa uchaguzi umekwisha, wasimame imara kuijenga nchi yao ya Kenya.
Rais mteule wa Kenya, William Ruto akizungumza na Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ofisini kwake, Karen, jijini Nairobi nchini Kenya
“Ndugu zangu Wakenya, tunawapongeza nyinyi kwa kuonyesha ukomavu wa demokrasia na kumaliza uchaguzi salama na leo tuko hapa pamoja kama Wakenya na wa-East Afrika tukishangilia uapisho wa Rais wetu mpya.
“Nataka niwaambie ndugu zetu Wakenya, kama kuna zawadi mliyoitoa kwa Afrika Mashariki mwaka huu, ni zawadi ya amani mliyoiweka katika uchaguzi. Tunawashukuru sana kwa zawadi hiyo muhimu,” amesema Rais Samia.