Refa Aliyechezesha Pambano la Mandonga Afunguka


BAADA ya matokeo ya pambano la Karim ‘Mandonga’ Said na Salim Abeid kufutwa, mwamuzi wa pambano hilo, Habib ‘Mkarafuu’ Mohammed amevunja ukimya na kueleza sababu za kutomhesabia Mandonga baada ya kupigwa na kuangushwa chini kama ambavyo kanuni zinasema.

Kwa mujibu wa kanuni za ngumi, bondia anapopigwa na kuangushwa, anahesabiwa hadi nane ili kuendelea, ingawa kwa Mandonga juzi usiku haikuwa hivyo hadi pale Rais wa Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBRC), Chaurembo Palasa aliponyanyuka na kutangaza kufuta matokeo ya pambano hilo lililochezwa Mtwara.

“Ni kweli nilipaswa kumhesabia Mandonga, lakini kabla ya kufanya hivyo mpinzani wake alipaswa kurudi kwenye neutral corner (kona huru), hakufanya hivyo, nilimuonya na kumtaka arudi, lakini ghafla alikuja tena alipo Mandonga na kurusha ngumi nyuma ya mgongo wangu.

“Wakati hayo yakiendelea tayari Mandonga alishakuwa sawa na kunyanyuka, hivyo sikuweza kumhesabia na pambano likaendelea,” alisema Mkarafuu ambaye pia ni mwenyekiti wa chama cha waamuzi wa ngumi za kulipwa.

Aliyewahi kuwa mwenyekiti na muasisi wa chama hicho, Ally Bakari ‘Champion’ alisema kiuhalisia, pambano hilo lilipaswa kuisha kwa Mandonga kupigwa kwa KO.

“Kama angemhesabia, Mandonga asingenyanyuka, alipaswa kuhesabu, lakini kama kulikuwa na figisu figisu fulani hivi na hata Palasa kufuta matokeo ya pambano hilo ni sahihi kabisa,” alisema Champion.

Siku hiyo pia, Twaha ‘Kiduku’ Kassim alimchapa kwa pointi Abdo Khaled wa Misri na kutetea ubingwa wa UBO Afrika kwenye uzani wa super middle wa pambano la raundi 10.

Licha ya ushindi huo, matokeo hayo yatamuongezea pointi kadhaa Mmisri ambaye amezichapa akiwa wa 257 duniani kulinganisha na Kiduku ambaye ni wa 92 akiwa na rekodi kubwa zaidi na uzoefu wa muda mrefu wa ulingo ambako amepigana mapambano 28 na la juzi lilikuwa la 29 na mpinzani wake amecheza mapambano 12.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad