Dhibiti sukari yako mwilini, ni kauli wanayotoa wataalamu wa afya juu ya namna ya kuepuka maradhi mbalimbali yanayoambatana na ugonjwa wa kisukari.
Kukatwa mguu au kiungo chochote cha mwili, kupoteza uoni pamoja na kukosa nguvu au hisia za kushiriki tendo la ndoa ni matokeo ya kuzidi kwa sukari mwilini.
Mfumo usio sahihi wa maisha, yaani kula bila kuzingatia mchanganyiko wa makundi matano ya chakula kama inavyoshauriwa na wataalamu na kufanya mazoezi pamoja na kupata muda wa kutosha kupumzika, ni kivutio cha ugonjwa huu kwenye miili ya watu.
Abeil Mashauri, mkazi wa Buza, Dar es Salaam ni kijana ambaye kwa zaidi ya miaka sita anasema alimuuguza baba yake ambaye sasa amefariki dunia kutokana na ugonjwa wa sukari.
“Hakuwa na uwezo wa kufanya jambo lolote, akipata jeraha ni ngumu kupona, kuna maeneo mengine alikuwa anasema anasikia ganzi kwa hiyo hata ukimchoma hasikii,” anaeleza.
Anaeleza umuhimu wa kutolewa elimu kwenye jamii namna ya kuzingatia lishe bora, ili kuepukana na kundi la magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo kisukari.
Wenye kisukari na hamu ya tendo la ndoa
Dk Kamu Kenneth kutoka Juda Polyclinic ya Temeke, Dar es Salaam akizungumzia namna ugonjwa wa kisukari unavyofifisha matumaini ya mtu kushiriki tendo la ndoa anasema, mtu anapokuwa na ugonjwa huo maana yake kiwango cha sukari kwenye damu kipo juu kuliko kiwango kinachohitajika.
Kiwango anachoeleza daktari huyo, ni kile kisichozidi saba kwa mtu ambaye hajala chakula na 11 kwa mtu aliyekula, akitahadharisha mtu atakapokuta kiwango chake cha sukari mwilini kipo 11 wakati hajala atahitajika kufuatiliwa mwenendo wake vyema kubaini kama ana ugonjwa wa sukari.
Hata kwa wale waliokula na kukuta sukari yao ipo juu ya 11, Dk Keneth anatadharisha kuwepo tatizo kwenye mwili wa mhusika, hivyo lazima mtaalamu aanze kufuatilia mwenendo sukari hiyo mwilini.
“Kwa mtu mwenye sukari maana yake ipo nyingi kwenye damu, inaathiri mzunguko wa damu, hivyo mishipa ya fahamu hairutubishwi,” anabainisha.
Kutokana na mishipa ya fahamu kutorutubishwa, Dk Kenneth anafafanua hali hiyo inasababisha mishipa hiyo kupoteza uhai wake.
“Mishipa ikishakufa hisia za mtu hushuka, sasa kinachotokea kwa mgonjwa wa kisukari si kwamba uume hausimami hapana…unasimama lakini hauwezi kusimama kwa kiwango ambacho mtu ataridhika, hivyo utafika wakati uume unasinyaa.
“Ili mtu asimamishe uume kwa muda mrefu lazima kiwango kikubwa cha damu kisukumwe, sasa kwa mgonjwa wa kisukari msukumo wa damu upo chini, hivyo mgonjwa hawezi kukaa muda mrefu akiwa amesimamisha uume,” anaeleza.
Kutokana na mishipa ya fahamu kufa kwa kukosa virutubishi, Dk Kenneth anaeleza hata uume wa mtu mwenye kisukari ukisimama hauwezi kupata hisia za kuendelea kushiriki tendo hilo, hali anayoitaja kuufanya uume usinyae zaidi.
Dk Kenneth anaweka wazi kuwa asilimia 35 hadi 75 ya wanaume wenye ugonjwa wa kisukari wanaishia kupata tatizo la kushindwa kusimamisha uume.
Anasema kuna wakati mtu mwenye ugonjwa wa kisukari hupata hisia za kushiriki tendo la ndoa, lakini anashindwa kutokana na mtiririko wa damu kuwa mdogo.
“Unakuta wengine wanatumia dawa aina ya Viagra wafanikishe kasi ya mtiriko wa damu mwilini ili ifike kwenye uume,” anabainisha.
Wanawake kukosa hisia
Kwa upande wa wanawake, Dk Kenneth anaeleza kinachotokea kwao mishipa ya fahamu inapoathiriwa na kukosa hisia, wakati akifanya tendo la ndoa majimaji hayazalishwi.
“Mwanamke mwenye kisukari huwa na ukavu ukeni, majimaji hayazalishwi kwa wingi kwa sababu hana hisia, hivyo akifanya tendo la ndoa hupata maumivu. Hali hiyo humfanya kutotamani kushiriki tendo hilo,” anasema.
Namna ya kuepuka hali hiyo
Dk Kenneth anasema njia pekee ya kuepukana na hali hiyo ni kudhibiti sukari mwilini. “Inabidi udhibiti chanzo, mfano kwa wale wanaotumia dawa za kuongeza nguvu za kiume hawatibu chanzo, ukipunguza sukari kwenye damu mtiririko wa damu unakuwa kawaida,” anasema.
Anaeleza ili wanaume au wanawake wenye tatizo la kisukari wasipitie changamoto ya kukosa hamu ya kushiriki tendo la ndoa, wanatakiwa kudhibiti sukari kwa kufanya mazoezi.
Dk Kenneth anasema, njia asilia ya kuondoa sukari kwenye damu ni kufanya mazoezi, ili kuitumia sukari iliyopo huku akisisitiza wanaovuta sigara au kunywa pombe waepukane navyo.
“Kitu kingine anachopaswa kukizingatia ni kupunguza vyakula vyenye mafuta. Mafuta huwa na tabia ya kwenda kuganda kwenye kuta za mirija ya damu, maana yake tundu linalopitisha damu linakuwa dogo, jambo ambalo husababisha mtiririko wa damu kuwa mdogo,” anasema.
Kuhusu sukari
Daktari kutoka Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Mbeya, Octavian Kasanga anasema watu wenye sukari huwa hawasimamishi uume, ndiyo maana hawashiriki tendo la ndoa.
Dk Kasanga anaeleza ili uume usimame kuna mawasiliano kati ya mfumo wa fahamu kwenye ubongo ambao husababisha kemikali mwilini kuzalishwa, kemikali hiyo ndio huchochea damu kwenda kujaa kwenye mishipa kwenye uume.
Damu hiyo inapojaa, Dk Kasanga anasema mishipa hiyo hufungwa, ili damu isirudi, hivyo hapo ndipo hutafsiriwa kuwa uume umesimama. Kwa mgonjwa wa kisukari anasema, mchakato huo wa kujaa damu kwenye mishipa ya uume na kufungwa ni changamoto kutokana na sukari kuathiri uwezo wa mishipa kusinyaa na kutanuka.
Nini ufanye kama una sukari
Anachoshauri Dk Kasanga kwa wagonjwa wa sukari, ni kuhakikisha sukari yao inakuwa sawa.
Dk Kasanga anasema mgonjwa hufanyiwa uchunguzi wa kina ili kutambua nini kimesababisha tatizo hilo, kwani wanaume wengi kwa sasa wana tatizo la uume kutokusimama na wengi si kwamba wana tatizo la sukari.
Anasema si kila mgonjwa wa kisukari mwenye tatizo la uume kutosimama sababu ni kisukari, bali kunaweza kuwa na sababu nyinginezo za kisaikolojia, hivyo ni muhimu mhusika kuonana na wataalamu kupatiwa ufumbuzi.
Aina za kisukari
Dk Kasanga anasema ugonjwa wa kisukari upo katika makundi kulingana na chanzo na matibabu yake, ambapo kwasasa yapo makundi mawili.
“Kuna aina ya kwanza na aina ya pili ya kisukari. Kundi la kwanza tunamaanisha kuna aina ya kisukari ambayo humpata mtu kuanzia utotoni au kumpata mtu kutokana na mwili kukosa insulin.
“Aina ya pili ya kisukari mtu anazaliwa ana insulin, lakini kemikali hiyo inapambana na changamoto ambazo mwili wa mtu haupokei vizuri insulin iliyopo, hivyo inaonekana kama haitoshelezi mwilini. Hii husababishwa na kutokufanya mazoezi na kutumia vyakula vyenye mafuta,” anasema.
Wagonjwa kutopona majeraha
Mtiririko mdogo wa damu ndio anaoutaja Dk Kenneth kuchangia majeraha wanayopata wagonjwa kutopona na wakati mwingine kuchukua muda mrefu kupona.
Anasema ili kidonda kipone lazima kirutubishwe na damu hutembea na virutubisho, akisema mtiririko mdogo mgonjwa anapopata jeraha mguuni mishipa ya fahamu huharibika kutokana na kukosa damu.
“Sasa mishipa ya fahamu ikiharibika kwenye miguu mgonjwa hata akikanyaga msumari hawezi kusikia maumivu yoyote, ndio maana wanashauri kuvaa viatu muda wote kwa sababu hawana hisia,” anaeleza.
Lishe kwa wenye kisukari
Ofisa Lishe Mtafiti kutoka Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC) Fatma Mwasora anasema mgonjwa anashauriwa kula mlo kamili uliotayarishwa kutokana na angalau chakula kimoja katika kila kundi la vyakula.
Pia ulaji wa kiasi kidogo wa vyakula aina ya wanga na sukari, kama vyakula vya nafaka mfano mkate, unga wa mahindi, wali, chapati, ulezi, mhogo,mtama na viazi.
“Aepuke nafaka zisizokobolewa kwa mfano dona, ngano au shayiri, vyakula kama sukari, glucose, asali, chokoleti, peremende, matunda ya kopo, tende kavu, ice cream, keki, biskuti na soda zote tamu, kwani sukari iliyoko kwenye vyakula hivyo huyeyushwa upesi tumboni na kusababisha sukari nyingi kwenye damu kwa muda mfupi,” anabainisha.
Aina nyingine ya vyakula anavyoshauri Fatma kutumika ni aina ya mbogamboga kwa wingi kwa mfano mchicha, matembele, karoti, majani ya maboga, kisamvu na mlenda, vyakula vya jamii ya mikunde kama mboga kuwa sehemu ya mlo wa siku, kwa mfano maharage, njegere, dengu, mbaazi, kunde na choroko.