Dar/mikoani. Wakati sintofahamu ikiibuka kutokana na maswali yanayoulizwa kwenye sensa ya majengo, likiwemo la kujua thamani ya nyumba, Serikali imetoa ufafanuzi kuwa lengo lake ni kupata taarifa za makazi yaliyopo nchini na kuona ni kwa kiasi gani yamekidhi viwango vilivyowekwa kimataifa.
Sensa hiyo ya majengo ilianza juzi na itafanyika nchi nzima ambapo maswali kadhaa yaliulizwa kwa wamiliki wa majengo kwa lengo la kupata taarifa muhimu za aina ya makazi, ubora na thamani yake.
Tofauti na ilivyokuwa kwenye sensa ya watu, baadhi ya wananchi wamekuwa wagumu kutoa ushirikiano kwa makarani katika sensa ya majengo kwa kile kinachohofiwa kuwa huenda kuna mpango usiofaa unapangwa na Serikali.
Jijini Dar es Salaam mmoja wa makarani katika Kata ya Tandika, Apenda Simon alisema amekutana na changamoto ya watu kukataa kutoa taarifa zinazohitajika kutokana na kuwa na wasiwasi.
“Unamuuliza mtu nyumba yako ina thamani gani, anakujibu Serikali inataka kujua thamani ya nyumba yangu ili iweje, kuna mpango gani mnataka kuja nao kiasi cha kutaka kujua thamani ya nyumba, kwa kifupi watu wamekuwa wazito, nadhani ni uelewa,” alisema Simon.
Mwananchi pia ilimshuhudia mwanamke mmoja aliyemtolea maneno makali karani baada ya kumpigia simu na kumhoji kuhusu nyumba yake.
“Siwezi kukutajia thamani ya nyumba yangu, nilishamalizana na Serikali nimenunua kiwanja, nimejenga nalipa kodi, sasa wanataka kujua habari za nyumba yangu za kazi gani,” alisikika mwanamke huyo.
Changamoto hiyo imeonekana pia mkoani Dodoma, ambapo makarani na wenyeviti wa mitaa wamesema wamepata changamoto za baadhi ya wamiliki wa nyumba kutokutoa ushirikiano wakiogopa kutozwa kodi kubwa au kunyang’anywa na Serikali.
Katibu wa wenyeviti Mkoa wa Dodoma ambaye pia ni Mwenyekiti wa Mtaa wa Sulungai, Gervas Lugunyale alisema katika mtaa wake kuna changamoto ya wamiliki wenye nyumba zaidi ya 10 kukataa kuandikisha taarifa zao kwa kuhofia kuchukuliwa nyumba zao na Serikali.
Alisema changamoto nyingine ni wamiliki hao kuogopa kutozwa kodi wakiamini taarifa hizo zitatumika.
Mkazi wa Mtaa wa Viwandani jijini Dodoma, Juma Matonya, alisema anaogopa nyumba yake kuhesabiwa kutokana na kodi na tozo kuwa nyingi kwa sasa.
“Kodi zinatutesa sana, tunaogopa maana sasa hivi kila kitu ni kodi, najua kuna baadhi ya wafanyabiashara, hasa wenye nyumba nyingi hawatatoa ushirikiano,” alisema Matonya.
Serikali yafafanua
Mwananchi lilimtafuta Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Dk Allan Kijazi, aliyetoa ufafanuzi wa suala hilo na kueleza nia ya Serikali ni njema katika suala hilo hivyo wananchi wasisite kutoa ushirikiano.
Kijazi alisema lengo ya sensa hiyo ni kujua hali ya kipato na uchumi wa wananchi na kipimo kikubwa katika hilo ni kuangalia makazi yao, ubora na thamani yake.
“Ili kujua hali ya uchumi wa mtu unaweza kuangalia kuanzia makazi yake, je anaweza kukidhi makazi ya aina gani. Hapa tunataka kuangalia ni kwa kiasi gani Watanzania wanaweza kukidhi makazi kwa viwango vya kimataifa.
“Tunategemea kupitia sensa hii ndio tupate taarifa hizi, hivyo ni muhimu kutoa ushirikiano na kujibu majibu sahihi kwa kuwa taarifa zinarekodiwa na ndiyo maana inasisitizwa kuwa wamiliki wa nyumba au wenye taarifa sahihi za nyumba ndio wajibu,” alisema Dk Kijazi.
Katibu Mkuu huyo alisisitiza umuhimu wa kutoa taarifa sahihi kwa kuwa ndizo zinazorekodiwa na zitatumika kama taarifa za awali endapo kutakuwa na shughuli zinazohusisha uhitaji wa taarifa hizo.
“Hili swali la thamani ya nyumba ni la kawaida tu, wewe mwenyewe uipe thamani nyumba yako, mfano ikitokea unataka kuiuza utaiuzaje au mradi umepita hapo hata kama tathmini ya kitaalamu itafanyika lakini wewe utakuwa umeonyesha thamani ya awali.
“Nafahamu hili limekuwa na maswali kwa kuwa ni mara ya kwanza kufanyika, tangu tupate uhuru hatujawahi kuwa na sensa ya makazi, niwatoe hofu dhamira ni njema kabisa, tunataka tujua aina ya makazi yetu,” alisema Dk Kijazi.
Mafanikio ya sensa
Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dk Albina Chuwa alisema hadi kufikia jana asubuhi watu waliohesabiwa walifikia asilimia 99.93 na wamebakiza asilimia 0.07 ya kaya zote nchini ambayo itaendelea kuhesabiwa hadi Septemba 5, mwaka huu.
Imeandikwa na Elizabeth Edward (Dar), Sharon Sauwa, Ramadhan Hassan, Mainda Mhando na Merciful Munuo (Dodoma).