Saida Karoli Afunguka Kutopata Chochote Kutokana na Wimbo wake wa Maria Salome Remix Uliofanywa na Diamond Platnumz



Unapozungumzia wasanii waliofanikiwa kutangaza utamaduni wa Mtanzania, jina la Saida Karoli huwezi kuacha kulitaja.

Msanii huyu alianza kupata umaarufu mwaka 2002 baada ya kuachia kibao chake cha ‘Maria Salome’ kilichopewa majina mengi ikiwemo Salome na ‘Kanichambu kama Karanga’ neno lililobeba jina la albamu yake ya kwanza.

Albamu hiyo ilikuwa na nyimbo nane ambazo nyingi aliziimba kwa lugha ya Kihaya na kati yake ni ‘Bakuba baizile’, ‘Alimu Atusile’, ‘Kaisiki part 1’, ‘Ndombo ya Solo’, ‘Iyondo’, ‘Oll njoka’, ‘Kaisiki part 2’ na ‘Maria Solome’ yenyewe.

Pamoja umaarufu alioupata ndani na nje ya nchi, msanii huyo hapo katikati alipotea mpaka pale alipoibuliwa tena na marehemu Ruge Mutahaba mwaka 2017 na kutoa kibao ‘Orugando’ ambacho hakikufanikiwa dkumrudisha mjini kama ilivyokuwa enzi za Maria Salome.

Africa, na wimbo wa kichaka aliowashirikisha wasnii Belle 9 na G Nako.

Mwananchi imefanya mahojiano na msanii huyu mahiri wa kucheza na kuimba, na kuzungumza mambo mbambalimbali ikiwemo kujua wapi alipo sasa,

alivyopokea kurudiwa kwa wimbo wake wa Maria Salome na msanii Diamond Platnumz na nini mikakati yake katika kuendeleza muziki wake.

Kwa sasa Saida anasema makazi yake yapo Buzurugwa jijini Mwanza na amekuwa anafanya kazi zake za muziki ambapo shoo nyingi huzifanya katika mikoa ya Kanda ya Ziwa, ingawa atakapohitajika anakwenda mkoa wowote kutoa burudani kulingana na makubaliano.

Wimbo wa Salome kurudiwa na Diamond


Akizungumzia kuhusu kurudiwa kwa wimbo wake wa Salome na msanii maarufu Diamond Platnumz ambaye alimshirikisha Rayvanny, Saida anasema ilikuwa ni jambo jema kwa kuwa aliona kazi aliyoifanya bado inathaminika na kutambuliwa.

Pamoja na hilo anasema kwa upande wa masilahi haukuwa nzuri kwake, lakini hakuwa na namna kwa kuwa kazi hiyo kwa mkataba alioingia ilikuwa chini ya uongozi wa FM Production.


“Nachokumbuka wakati wimbo huu unataka kuachiwa aliyenipigia simu alikuwa Diamond mwenyewe na kuniomba kuwa nimpe ruhusa arudie wimbo huo, na mara baada ya kuongea naye siku hiyo hiyo jioni ukaachiwa.

“Ilinishangaza nikajua wakati ananiomba labda walikuwa bado katika maandalizi ya kuiandaa, lakini ndio hivyo kumbe walikuwa wameshakamilisha kila kitu, sikuwa na namna kwa kuwa haikuwa chini yangu tena kutokana na mkataba ambao niliingia na FM,”anasema Saida.

Mwananchi ilitaka kujua ni kiasi gani cha fedha alipatiwa baada ya kutoka kwa remix ya wimbo huo, lakini msanii huyu hakuwa tayari kuweka wazi zaidi ya kusema fedha aliyoipewa haikuzidi Sh1 milioni.

Hata hivyo wakati wimbo huo video yake mpaka sasa ikiwa imetazamwa mara milioni 39 kwenye mtandao wa YouTube, tangu ulipoachiwa mwaka 2015, Saida anasema hakuna anachoambulia licha ya kutamani angekuwa anapata japo kidogo.

“Siwezi kulaumu kwa yaliyotokea wakati ule, japokuwa kibinadamu inaumiza kuona kuna wanaofaidi kupitia jasho lako, lakini naomba hii iwe funzo kwa wasanii wengine na wale wanaotaka kuingia kwenye usanii katika suala zima la mikataba,tuisome mara mbili mbili.

“Usiangalie tu umepangishiwa nyumba ya gharama kubwa, kupewa usafiri wa gharama ukaona maisha umeyapatia, hawa hawa wanaotusimamia wakati mwingine hutumwaga.

”Tumeshuhudia wengine hata wakishinda kupaza sauti kuomba msaada pale wanapokumbwa na matatizo mbalimbali ikiwemo kuumwa kwa kuwa awali walikuwa wakiishi maisha yasiyo ya kwao,”anasema Saida ambaye ni mama wa watoto watano.

Saida pia aliiomba Serikali kuingilia kati suala hilo la mikataba ikiwemo kuweka sheria kushinikiza mikataba iandikwe kwa lugha ya Kiswahili ili iwe rahisi kueleweka.

Nini alichonufaika kupitia albamu ya ‘Kanichambua ‘kama karanga’

Saida anasema akizungumzia alichofaidika katika albamu ya Salome, sio kihivyo kama ilivyokuwa kwa ukubwa masikioni na machoni mwa watu.

‘Naweza kusema zaidi ya kupata umaarufu kikubwa nilichoambulia ni gari aina ya carina yenye thamani ya Sh5 milioni, ambayo hata hivyo mwisho wa siku ilinishinda hata fedha za kuifanyia matengezo, nikaona niiuze kwa bei ya kutupwa ambayo ni aibu hata kuitaja gazetini,”anasema Saida.

Faida nyingine aliyoipata, msanii huyu anasema ni kuzunguka maeneo mbalimbali ndani na nje ya nchi.

Hata hivyo pamoja na kuwa na shoo nyingi, Saida anasema alichokuwa akiambulia ni kidogo kuliko alichokuwa anaingiza kwa kuwa hela ilikuwa ikipita kwenye mikono ya watu wengi.

“Hata hii nyumba ninayoishi, nimejenga kwa fedha za shoo nilizokuwa ninafanya mwenyewe, siyo zile za wakati nipo juu kimuziki,”anasema.

Katika hili anasema hatamsahau marehemu Ruge kwani wakati wa kutaka kurudi kwenye muziki, alimwambia sasa angependa aimbe kwa kujitegemea mwenyewe jambo ambalo alimfanikishia, lakini ndio hivyo haikuisha miaka mitatu akafariki.

Tofauti ya muziki enzi zao na sasa

Anasema muziki wa zamani licha ya mapato kuwa mengi, lakini msanii alikuwa akipata kidogo kutokana na kuwepo kwa mapromota waliotanguliza zaidi masilahi yao.

Nini mipango yake

Saida anasema moja ya mipango yake ni kuwa na vyombo vya bendi, kwani kwa sasa kutokana na kutokuwa na vyombo hivyo akitakiwa kupiga live inabidi kukodi.

Anasema akivikodi inabidi akodi na wapigaji jambo linalomuongezea gharama, hivyo kukosa kazi nyingi kutokana na ukubwa wa bei unaowashinda wateja. “Nimerekodi midundo ya nyimbo zangu nikipata shoo huicheza na kuimba, jambo linalopunguza ile ladha na maana nzima ya muziki wa ‘live’,”anasema.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad