Saini ya Zumaridi yaibua utata kortini



SAINI inayodaiwa kuwa ya Diana Bundala maarufu  Mfalme Zumaridi, jana ilizua utata katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Mwanza, baada ya kudaiwa imeghushiwa na askari aliyechukua maelezo ya onyo.

Askari huyo ambaye ni shahidi wa upande wa mashtaka katika kesi inayomkabili Zumaridi na wenzake 84, Joseph Robert, amedaiwa kughushi saini ya Zumaridi ambaye ni mshtakiwa namba moja.

Shahidi huyo anadaiwa kughushi saini katika kielelezo cha maelezo ya onyo kilichofikishwa mahakamani kwa ajili ya kutumiwa kama sehemu ya ushahidi mbele ya kesi hiyo inayosikilizwa na Hakimu Mkazi Crescensia Mushi.

Alidai kuwa mshtakiwa namba moja alikiri makosa yake katika kituo cha polisi na kutia saini katika maelezo ya onyo kituoni hapo na kuomba maelezo hayo yapokewe na mahakama kama kielelezo na sehemu ya ushahidi wa kesi hiyo.

Hata hivyo, Wakili wa Utetezi, Erick Mutta, alipinga maelezo hayo kutumika kama kielelezo katika kesi hiyo, huku akidai kuwa aliyetia saini katika maelezo hayo si mshtakiwa bali saini yake imeghushiwa.


Wakili Mutta alidai kuwa mshtakiwa alipigwa kabla ya kuchukuliwa maelezo na kuongeza kuwa maelezo hayo yalichukuliwa nje ya muda kwa kuwa yalichukuliwa dakika 30 kabla, hivyo aliiomba mahakama kulinganisha saini ya mshtakiwa iliyoko katika maelezo hayo na ile iliyopo katika vitambulisho vyake.

Wakili Mutta pia aliiomba mahakama kuweka madai hayo katika maandishi ya kimahakama ili kusaidia katika uamuzi.

Wakili wa upande wa mashtaka, Dorcas Akyoo, alipinga ombi hilo na kudai kuwa saini za mtu zinaweza kuwa zaidi ya moja, hivyo kuomba aulizwe mhusika ambaye ni mshtakiwa kwa kuwa alikuwapo mahakamani.


Mshtakiwa huyo alipoulizwa na mawakili wake juu ya maelezo hayo, alidai kuwa saini hiyo si yake bali imeghushiwa.

Kutokana na utata huo, Hakimu Mushi aliahirisha kesi hiyo hadi Septemba 19, mwaka huu, huku akiutaka upande wa utetezi kuleta ushahidi na vielelezo vitakavyobainisha ukweli wa madai hayo.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad