RAIS Samia Suluhu Hassan amesema mkutano wa Bunge unaofanyika mwezi huu utapitisha muswada wa sheria kuanzisha bima ya afya kwa wote.
Mkutano huo umepangwa kuanza Jumatatu jijini Dodoma. Rais Samia alisema hayo Jumapili kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam wakati wa Jubilei ya miaka 50 ya Umoja wa Wanawake Wakatoliki Tanzania (WAWATA).
Rais Samia Suluhu akiwa na viongozi wa dini kwenye maadhimisho ya Jubilei ya miaka 50 ya Umoja wa Wanawake Wakatoliki Tanzania (WAWATA).
“Niwaombe sana tutakapopitisha sheria hii watanzania tukaijunge na mifuko ya bima. Nawapa uhakika tunajua udhaifu uliopo kwenye mifuko yetu ya bima,” alisema.
Rais alisema anafahamu udhaifu uliopo kwenye mifuko ya bima na hatua zimechukuliwa hivyo utakaoanzishwa utakuwa madhubuti wenye sheria na kanuni zitakazowezesha watu wote watibiwe.
“Mfuko huu utahakikisha mtu anapata matibabu yote anayopaswa kupata. Huu ni kama upatu ambao Watanzania wote tunakwenda kucheza upatu huo na kati yetu anayepatwa na shida, upatu huo unamsaidia,” alisema.
Aliongeza; “Ni kupitia bima ya afya kwa wote ndipo tutaweza kutoa matibabu kwa kila Mtanzania anayeishi ndani ya nchi yetu,”
Pia Samia alitoa maagizo sita kwa wanawake kuhakikisha wanayasimamia na kutekeleza yakiwemo ya kusimamia maadili, kulinda na kulea watoto, kushiriki shughuli za kiuchumi, kudhibiti unyanyasaji wa kijinsia lakini pia kutoogopa kushiriki katika siasa.
Aliwataka wanawake wazingatie maandiko ya vitabu vya dini yanayompatia heshima, ushujaa na hamasa mwanamke kuwa mstari wa mbele kusimamia masuala mbalimbali katika jamii yakiwemo maadili.
Rais Samia alisema kwa sasa kinachozungumziwa ni maporomoko ya maadili kwa vijana, kazi ambayo wanawake wamepewa kuwasimamia vijana hadi wavielewe vitabu hivyo vya dini na kusimamia maadili.
Alisema wanawake wamepewa kazi hiyo kwa sababau vitabu vya dini vinamtambua mwanamke kuwa ni mtu anayefumbua kinywa chake kwa
hekima, nidhamu na ulimu wake umejaa mafundisho mema.
“Wanawake ni jeshi kubwa na jeshi maana yake hulinda himaya yake hulinda nchi yake sisi wanawake ni jeshi lakini hatutafanya kazi hii pekee yetu akina baba na jamii kwa ujumla watatusaidia,” alisema Rais Samia.
Aidha, alizungumzia suala la wanawake kupatiwa elimu ya uongozi ili kuwajengea kujiamini na kuwa na uthubutu wa kukabili changamoto.
Alinukuu kitabu cha dini kilichoeleza kuwa mwanamke anatakiwa kuwa jasiri, asiogope wala kukata tamaa kwa kuwa Mungu yupo naye pia mwanamke amevishwa nguo ya ushupavu na heshima na hucheka bila kuogopa yajao.
“Nawaomba wanawake wenzangu kupitia Wawata na makundi yeyote ya dini twendeni kifua mbele tukafundishane, tukalindane na tukalinde watoto wetu, maana sisi ni mashujaa tuna heshima na mwenyezi Mungu yupo nasi,” alisema Rais Samia.
Aliwataka wanawake wakajichunguze na kujikagua kama bado wamebaki na heshima na ushujaa waliokabidhiwa na mwenyezi Mungu ili na wao waweze kuifundisha jamii iwe na maadili na maendeleo.
Rais Samia aliwataka wanawake nchini kuongeza jitihada katika shughuli za kiuchumi hasa ndogo zinazowapatia kipato na serikali itawasaidia wafanye vizuri.
Aliipongeza Wawata kwa kuwa mstari wa mbele kufundisha wanawake kuhusu ujasiriamali na namna ya mwanamke kujiingizia kipato.
Aidha, Rais Samia aliwataka wanawake kushiriki kikamilifu bila woga katika kuwania nafasi za uongozi na ngazi za uamuzi.
Alisema serikali inatoa nafasi maalumu za ushiriki wa wanawake na kuwasisitizia wasiogope kuwania nafasi hizo.
Kwa upande wa mabadiliko ya sayansi na teknolojia, alisema dunia ya sasa inakwenda kwa kasi na teknolojia ni silaha ya vijana.
Aliwataka wanawake, akina baba na wazazi kwa ujumla kuwaelekeza vijana matumizi sahihi ya teknolojia hiyo ili kuepuka kujiingiza katika mambo yasizoendana na maadili na utamaduni wa mtanzania.
“Sisi serikali na taasisi za wanawake tushirikiane kuyafanyia kazi ili tuwe na jamii ambayo itaiendeleza nchi yetu itazishika dini zetu na kuifanya Tanzania iwe mahali salama kuishi na yenye vijana wenye maadili,” alisema Rais Samia.
Pia, aliagiza wanawake kushiriki katika vita dhidi ya unyanyasaji wa kijinsia akitilia mkazo unyanyasaji wa pande zote wanawake na wanaume.
Awali, Mwenyekiti wa umoja huo, Evelyne Mtenga aliomba serikali isaidie kuhakikisha bima ya afya inawafikia wengi hasa wanawake waishio vijijini.
Mtenga alisema kwa sasa bado idadi kubwa ya watanzania hususani wanawake hawajafikia huduma hiyo ya bima ya afya.
“Tunaiomba serikali kuona namna ya kusaidia makundi maalumu kupata bima nafuu ili kuwa na uhakika wa kupata bima ya afya,” alisema.
Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Askofu Mkuu Gervas Nyaisonga alisema katika miaka hiyo 50 ya Jubilee yameshuhudiwa mafanikio ya akinamama katika nyanja mbalimbali.
“Mama zetu wanakusudia kufanya mambo mengi wanatambua kuwa ukimwezesha mwanamke mmoja unawezesha watu wengi zaidi. Tunakuomba Rais uendelee kuwa karibu na wanawake nchini. Uendelee kusimama kidete kupambana na vitendo vyote vya ukatili vya unyanyasaji dhidi ya wanawake na watoto,” alisema Askofu Mkuu Nyaisonga.