Ndani ya miezi 14, tozo za miamala ya kielektroniki zimerekebishwa mara tatu kutokana na malalamiko ya wananchi, jambo linaloelezwa kuwa ni udhaifu katika utekelezaji wa sera na mipango ya maendeleo katika Taifa.
Makato hayo yaliyotambulishwa na Sheria ya Fedha ya mwaka 2021 kama tozo za miamala ya simu na kuanza kutekelezwa Julai 15 mwaka jana yalizua malalamiko, hali iliyomlazimu Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kuitisha kikao cha dharura na mawaziri wake waliokubaliana kupunguza viwango.
Kutokana na kikao hicho, ukomo wa tozo hizo ulipunguzwa mpaka Sh7,000 kwa miamala inayozidi Sh3 milioni kutoka Sh10,000 ya awali. Hata hivyo, malalamiko hayakukoma na Serikali ikapunguza tena hivi karibuni.
Kwenye Bunge la bajeti lililohitimishwa Juni 30, Serikali ilishusha ukomo huo kutoka Sh7,000 mpaka Sh4,000, lakini ikatanua wigo kwa kuihusisha miamala yote inayofanywa kielektroniki, kuanzia benki mpaka simu za mkononi na intaneti. Kelele zimekuwa kubwa na kuwalazimu mawaziri wanne kujitokeza kufafanua malengo ya kuanzisha tozo hizo.
Kelele zilizotolewa na wananchi, watoa huduma za fedha, mawakala na wafanyabiashara pamoja na wafanyakazi, zimeilazimu Serikali kurudi mezani na kuzipitia Kanuni za Tozo za Miamala ya Kielektroniki ya mwaka 2022 na kufuta baadhi ya vipengele sambamba na kupunguza kiwango cha makato kati ya asilimia 10 mpaka 50.
“Ni mabadiliko mengi yaliyofanywa ndani ya muda mfupi. Nadhani watendaji watakuwa wamejifunza umuhimu wa kuwashirikisha wananchi kuanzisha vitu vipya watakavyoviunga mkono kuepuka hali hii. Hapa mapato yaliyokusudiwa hayawezi kupatikana, ni hasara kwa Serikali yenyewe,” anasema Hanifa Chiki, ofisa utawala wa kampuni binafsi jijini Tanga.
Ukiwasikiliza viongozi wa Serikali hata chama tawala, anasema muda mwingi wanasisitiza halmashauri kuwashirikisha wananchi katika kuibua miradi, lakini udhaifu huo unajidhihirisha kwenye mambo kama hili la tozo za miamala.
“Vyombo vya habari viliripoti kuhusu miradi ya mabilioni ya shilingi iliyosuswa na wananchi maeneo tofauti. CAG (Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali) ameionyesha na sababu ni kutowashirikisha wananchi, hili la tozo nalo linaangukia kwenye kundi hilo. Serikali ijifunze, kuanzia juu mpaka kijijini,” anasisitiza Hanifa.
Mtaalamu wa sera
Kutokana na mabadiliko ambayo Serikali imelazimika kuyafanya kwenye tozo hizi ambazo viwango vipya vinatarajiwa kuanza Oktoba mosi, Profesa Humphrey Moshi, mtafiti mbobezi wa masuala ya sera anasema kilichotokea ni matokeo ya uandaaji wa sera bila kufanya utafiti wa kina.
Profesa huyu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) anasema kodi ni suala la lazima kwa wananchi kulipa, lakini inatakiwa kuzingatia mbinu sahihi za uandaaji wake ili kutoleta malalamiko kwa umma.
Msomi huyu anasema bila kuwa na sera sahihi inayoeleweka na kuungwa mkono na wananchi, ni rahisi mambo kugoma hivyo ni jukumu la Serikali kuhakikisha misingi inazingatiwa.
Anasema sera ni taarifa ya Serikali kwa wananchi wake inayoonyesha namna itakavyoshughulikia changamoto iliyopo na katika uandaaji, mbinu kuu mbili hutumika ambazo ni ile inayotegemea ushahidi na inayozingatia maoni.
Sera inayozingatia ushahidi anasema hutumia matokeo ya utafiti, kuunganisha malengo yake na taasisi, kuwashirikisha wadau, kuhoji mazingira, mbinu za ufuatiliaji, kuonyesha mianya huku ikiwa na maono mapana.
“Mbinu hii ilianza kutekelezwa miaka ya 1990 nchini Uingereza, Tony Blair akiwa waziri mkuu. Inaamini katika ushahidi wa kiutafiti ili kuwa na matokeo chanya,” anasema Profesa Moshi.
Kuhusu sera inayozingatia maoni, Profesa Moshi, anayeunga mkono umuhimu wa tozo katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo anasema hulinda zaidi maslahi ya kisiasa bila kuhitaji ushahidi wa kitafiti.
“Ukiangalia hili la tozo, hapakuwa na utafiti wala ushirikishaji wa wadau ambao wasingeweza kulalamika baadaye iwapo wangeshirikishwa tangu mwanzo, hakuna malengo ya muda mrefu. Tozo lazima ziwe himilivu, kila kundi lilipe kodi kulingana na kipato chake,” anashauri.
Iwapo utafiti na ushirikishaji wananchi utafanywa, msomi huyu anasema utekelezaji unaweza kukwama iwapo kutakuwa na sababu zilizo nje ya uwezo wa udhibiti wa binadamu.
“Sera yako ikihamasisha kilimo kisicho cha umwagiliaji, mvua zisiponyesha utekelezaji utakwama,” anafafanua.
Mageuzi ya kidijitali
Tozo hizi zinazolalamikiwa zimeanzishwa katika kipindi ambacho Serikali inahamasisha uchumi wa kidijitali unaohitaji malipo ya kielektroniki tofauti na ya fedha taslimu ambao ni mgumu kuufuatilia na kukusanya mapato ya kutekeleza mipango ya umma.
Ukusanyaji wa tozo hizi unaelezwa kuwakatisha tamaa wananchi kufanya miamala ya kidijitali kama ilivyoelezwa na kampuni ya Vodacom kwamba katika robo ya kwanza mwaka huu mapato yake ya huduma za Mpesa yalipungua kwa zaidi ya Sh100 bilioni.
Profesa Abel Kinyondo wa UDSM anasema kama tunahamasisha kuhamia uchumi wa kidijitali basi gharama zinapaswa kuwa chini kwani kuweka tozo ni kudumaza malengo hayo japokuwa kodi haikwepeki ila kila kundi ligushwe kulingana na uwezo wake.
Mkurugenzi Mtendaji wa Repoa, Dk Donald Mmari anasema jicho la mataifa mengi duniani kwa sasa limejielekeza katika vyanzo vya mapato ya kidijitali.
“Dunia ndio inaelekea huko, kabla ya kuibuka kwa ugonjwa wa Uviko-19 kwa mfano, mchango wa biashara za mtandaoni duniani ulikuwa asilimia 10 tu lakini mwaka huu umeongekeza hadi asilimia 20. Kuna shughuli nyingi zinahamia huko kwa hiyo ni eneo muhimu lisiloepukika,” anasema Dk Mmari.
Hata hivyo, anakumbusha kuwa “jambo la msingi ni kuhakikisha tunafanya utafiti ili tukusanye kodi huko bila kuathiri uwekezaji wake.”
Utayari wa wananchi
Kuanzia Oktoba mosi Watanzania wataanza kutozwa viwango tofauti vya tozo ya miamala ya kielektroniki baada ya Serikali kutangaza kuvifanyia marekebisho, huku ifuta katika baadhi ya maeneo, ikiwamo ile ya kuhamisha fedha kutoka benki kwenda kwenye simu au kinyume chake, kuhamisha fedha kutoka akaunti moja kwenda nyingine au kutoka benki moja kwenda benki nyingine.
Kwenye ufafanuzi ilioutoa, Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), ilisema Sh117 bilioni zilizokusanywa mwaka 2021/22 zilitumika kujenga vituo vya afya 234, hivyo kuwataka wananchi kuendelea kuchangia utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Kuhusu utayari wa kulipa kodi, wananchi wanasema wapo tayari kufanya hivyo, ila kuwe na usawa kulingana na kipato cha kila mmoja.
“Kama ninaweza kuchangia harusi ya rafiki yangu anayeoa, kwa nini nisichangie maendeleo? Tatizo hakuna usawa, mamalishe analipaje tozo sawa na mfanyabiashara mkubwa?” anahoji James Mashasi, mkazi wa Kinyerezi, jijini Dar es Salaam.
Abdulfatah Lyeme naye anasema “kuna Mtanzania anatuma Sh5,000 kijijini kwao halafu Serikali inakata tozo, hata kama inajenga shule huyu hawezi kufurahia, ndio maana waliolalamika ni watu wa hali ya chini.”
Profesa Kinyondo anasema utafiti walioufanya mwaka 2019 na 2020 katika mikoa ya Mtwara na Lindi ulionyesha asilimia kubwa ya wananchi wako tayari kulipa kodi ili mapato yatumike kwenye miradi ya kitaifa, lakini wangependa kuona inagusa maisha yao.
“Tandale wakilipa tozo ijenge madarasa ya Songea haiwagusi sana wao, ni muhimu sana kuchangia maendeleo ya kitaifa, lakini angalau asilimia tano iwe inapelekwa chini kwa wananchi waliotoa,” anashauri Profesa Kinyondo.
Profesa Kinyondo anasema hata matamko ya viongozi kwenye uzinduzi wa miradi ya maendeleo huonekana kuwatenga wananchi, jambo linalowapunguzia ari ya kujitoa zaidi kuchangia mapato ya Serikali.
“Kwa mfano tukikusanya kodi halafu tukawaambia tozo zenu hizi ziliwezesha mambo haya badala ya kusema ‘Serikali inajenga au CCM imejenga’ hii itasaidia kuwapa umiliki, watajisikia vizuri na watapenda kuchangia zaidi,” anakumbusha.
DavidGraysonKazuva
2h
Haswa ccm wanapojisifia kuwa, ccm imefanya mambo kadhaa wa kadhaa wakati ni wananchi wote waliotozwa kodi na tozo zinazoumiza. Kwa mfano, wamejimilikisha viwanja vya mpira nchini, wakati kipindi hicho vinajengwa, wanachama wa iliyokuwa tanu na asp na hata baada ya kufanywa ccm, walikuwa wachache mno, wasingeweza kuvigharamia katika kuvijenga. Kodi za wanamchi wote ndio zilizojenga, ila kwa udhalimu wao wa siku zote, leo viwanja hivyo ni mali yao. Nashangaa hadi leo wanaendelea kuburidika maofisini wakati watu wa chini wameumia vya kutosha kwa tozo na kodi za kukatwa mara mbilibili kinyume kabisa na sheria na kanuni husika. Hapo hapo tunaambiwa mikopo ya uvico inafanya hayo hayo ambayo tozo zinadaiwa kufanywa!!Zaidi