SERIKALI imesema haina kesi 1,097 za kodi za muda mrefu zenye thamani ya Sh. trilioni 360 na dola za Marekani milioni 181.4 ambazo hazijaamuliwa huku Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) akifafanua kuhusu suala hilo.
Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Mwigulu Nchemba.
Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Mwigulu Nchemba alitoa kauli hiyo bungeni jana alipojibu swali la Mbunge wa Kisesa (CCM), Luhaga Mpina ambalo juzi Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson aliagiza lijibiwe upya.
Dk. Nchemba alisema hadi Agosti mwaka huu kulikuwa na mashauri 854 kwenye hatua mbalimbali za usikilizaji yenye kodi inayobishaniwa ya Sh. trilioni 4.21 na dola za Marekani milioni 3.48 katika Bodi ya Rufani za Kodi na Baraza la Rufani za Kodi.
Katika swali la nyongeza, Mpina alisema kwa mujibu wa taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa mwaka 2019/20 na mwaka 2020/21, kesi alizotaja zimesajiliwa kwenye baraza la rufani za kodi na bodi ya rufani za kodi.
“Zipo taarifa za uhakika kwa mwaka huu wa fedha serikali iliamua kupokea Sh. bilioni 700 kupitia kesi hizo za Sh. trilioni 360 na Desemba 2021 hadi Februari 2022 serikali ilipokea fedha hizo na kufuta kesi zenye thamani ya Sh. trilioni 360, kwanini serikali iliamua kupokea fedha Sh. bilioni 700 badala ya Sh. trilioni 360 kama madai halali ya nchi?”alihoji.
Waziri Mwigulu alikiri taarifa za CAG kuonyesha hilo na kwamba kilichofanyika baada ya mzozo wa Acacia na serikali, jambo hilo lilipelekwa kwa Kampuni ya Barrick.
“Kipindi cha Hayati Magufuli aliunda timu ya kufanya makubaliano na yaliendelea kwenye mjadala na yaliisha Januari 2020 na Tanzania ilikubali kuacha Sh. trilioni 360 na kupokea kiasi hicho na kuunda Kampuni ya Twiga ambayo ina ubia wa asilimia 16 kwa serikali na asilimia 84 kwa Barrick,” alisema.
Alisema kuwa mengine yaliyokubaliana mbali na ubia kulikuwa na kesi kati yao na serikali ya dola za Marekani bilioni 2.7 wakafuta na walikubaliana kutoa dola za Marekani milioni 40 kwa ajili ya ujenzi wa barabara.
Alisema walikubaliana watakuwa wanatoa dola za Marekani milioni 10 za ujenzi wa maabara ya madini.
“Kilichofuatia mwaka 2021 tulipokea gawio na mwaka 2022 tulipokea gawio na dola Milioni 300 ambazo ni Sh. bilioni 700, ilikuwa ni sehemu ya makubaliano kwenye mjadala na sherehe ile ilifanyika Ikulu mbele ya Hayati Magufuli,” alisema.
JICHO LA CAG
Katika ripoti yake ya ukaguzi kwa mwaka 2020/21 iliyowasilishwa bungeni Aprili 12 mwaka huu, CAG Charles Kichere ameligusia suala hilo, akisema hesabu za Mamlaka ya Mapato (TRA) kwa mwaka wa fedha 2020/21 zinaonyesha kuwapo kodi zilizoshikiliwa katika mahakama za rufani kwa muda mrefu Sh. 357,308,998,541,722 (Sh. trilioni 357.309).
Anabainisha kesi 46 za kodi zenye thamani ya Sh. 724,183,356,570 (Sh. bilioni 724.183) zipo katika Mahakama ya Rufani kwa mwaka 2020 na 2021.
"Katika mwaka wa fedha 2018 hadi 2021, kuna idadi ya kesi 176 zenye thamani ya Sh. 1,176,301,825,259 (Sh. trilioni 1.176) katika Mahakama ya Rufaa ya Mapato ya Kodi (TRAT)
"Kesi 847 zenye thamani ya Sh. 355,408,513,359,893 (Sh. trilioni 355.308) zipo katika Bodi ya Rufani ya Mapato ya Kodi (TRAB) za tangu mwaka 2016 hadi 2021. Mwaka 2017 ilikuwa na kiasi kikubwa cha kodi ya Sh. 349,862,963,907,128 (Sh. trilioni 349.863).
"Katika majadiliano niliyofanya ya tarehe 23 Septemba 2021 na TRAB pamoja na TRAT, nilibaini changamoto katika utaratibu wa kusikiliza kesi," anasema CAG na kuzitaja shida hizo zinajumuisha upungufu bajeti uliokwamisha usikilizaji na kufanya uamuzi kwa kesi hizo kwa muda.
CAG anasema kuna rufani za kesi za kikodi 45 zenye thamani ya Sh. 5,594,675,387,242.4 (Sh. trilioni 5.595) na kesi tisa (9) zenye thamani ya Sh. 56,678,445,387.80 (Sh. bilioni 56.678) zilizopo TRAT na TRAB mtawalia.
Anasema ingawa rufani hizo za kesi za kikosi zilikuwa katika mazungumzo (negotiations) kati ya serikali na walipakodi, mazungumzo hayo yamechukua muda mrefu bila kufikia mwafaka.
"Kutokana na majibu ya TRA, hadi kufikia tarehe 31 Desemba 2021, hali za kesi katika mahakama za rufani za kikodi zipo kesi 866 zenye thamani ya Sh. 5,190,108,141,768 (Sh. trilioni 5.19) zinazohusisha dola za Marekani 248,397,084 zilizobadilishwa kwa Sh. 2,309.24 kwa dola.
"Miongoni mwa kesi za rufani zilizoisha ni kesi 45 zenye thamani ya Sh. 5,594,675,387,242.40 (Sh. trilioni 5.595) ambazo zipo katika mazungumzo kati ya serikali na
kampuni za madini ambayo ni North Mara Gold Mine, Pangea Minerals Limited, Bulyanhulu Gold Mine na ABG Exploration.
"Kuna kesi Na.189 ya mwaka 2017 inayoihusu Bulyanhulu Gold Mine imepinga uamuzi wa kulipa kiwango pungufu cha Sh. 21,395,712,853,964 (Sh. trilioni 21.396) ili kusajili pingamizi la kodi kwa tathmini ya kodi kutokana na kutokuwa na taarifa za walipakodi (Jeopardy Assessment) kwa mwaka 2000-2017 kati ya jumla ya deni la Sh. trilioni 343.5. Kesi hii imetolewa mahakama za rufani za kikodi na kurejeshwa kusikilizwa na TRA," anafafanua.
CAG anaishauri serikali iharakishe mazungumzo (negotiations) na
walipakodi kwa kesi zilizo katika mazungumzo," CAG Kichere anawasilisha.