Serikali yafafanua malipo kwa mstaafu aliyefariki




Profesa Joyce Ndalichako
SERIKALI imesema malipo ya mafao kwa mstaafu aliyefariki dunia huzingatia kanuni zilizopo na ikitokea amefariki mfuko hulipa mafao ya mkupuo, jumla ya pensheni ya miezi 36 sawa na miaka mitatu kwa wategemezi.

Hayo yalibainishwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Profesa Joyce Ndalichako bungeni Jumanne wakati akijibu swali la Mbunge wa Ulyankulu, Rehema Migila (CCM).

Migila katika swali lake alitaka kufahamu mpango uliopo wa kuwapatia warithi wa mstaafu asilimia 67 ya michango yake anapofariki dunia.

Akijibu swali hilo, Profesa Ndalichako alisema Mfuko ya Hifadhi ya Jamii hutoa mafao kwa wanachama wake kwa mujibu wa Sheria ya Hifadhi ya Jamii Sura Namba 135 kama ilivyorejewa kupitia Sheria ya Marekebisho ya Sheria Namba 6 ya mwaka 2019 ambapo fao la warithi ni mojawapo ya mafao yanayotolewa mwanachama anapofariki.


Alisema kwa upande wa mfuko wa PSSSF, kupitia Kifungu cha 39(1) cha Sheria ya Mfuko mstaafu anapofariki hulipa mafao ya mkupuo ambayo ni jumla ya pensheni ya miezi 36 sawa na miaka mitatu kwa wategemezi.

Profesa Ndalichako alisema kwa upande wa NSSF, kwa mujibu wa Kifungu cha 37 (1) (2) (3) cha Sheria ya Mfuko, mstaafu anapofariki, hulipa mafao ya mkupuo sawa na pensheni ya miezi 24 kwa wategemezi.

Alisema ulipaji wa mafao huzingatia Sheria ya Hifadhi ya Jamii ya mwaka 2018 na marekebisho yake ya mwaka 2019 na Kanuni za Mafao za mwaka 2018 kama zilivyorejewa mwaka 2022.


Mafao yanayolipwa hayazingatii asilimia ya michango isipokuwa wastaafu na wategemezi hulipwa mafao kulingana na kanuni zinazoongoza ulipaji wa mafao ya pensheni.

Profesa Ndalichako alisema pia suala la kuongeza kiwango cha mafao kwa wastaafu mifuko imekuwa na utaratibu wa kufanya tathmini nakuona namna gani itaweza kuongeza mafao hayo.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad