SI Yanga pekee inayopiga hesabu za kukutana na Al Hilal ya Sudan hata wao huko walipo ni kama wameshaivuka St Georges wanaiwaza Yanga.
Yanga inacheza mechi mbili nyumbani dhidi ya Zalan ya Sudan Kusini ambazo wanajipa nafasi kubwa ya kushinda na sasa hesabu zao zipo kwa Al Hilal wanaonolewa na Florent Ibenge raia wa DR Congo mwenye uzoefu na soka la Afrika.
Ibenge ambaye amewekeza kwenye usajili mkubwa kama ilivyo Yanga, alisema kikosi cha Yanga chasasa kina mastaa ambao amewahi kufanya nao kazi na mahiri haswa Fiston Mayele aliyeko katika kiwango bora.
“Namfahamu Fiston (Mayele) nimefanya naye kazi ni kijana wangu lakini bahati mbaya kwetu tunakwenda kukutana naye akiwa katika kiwango bora sana tutahitajika kuwa naye makini kama tukikutana,”alisema Ibenge ambaye hajawahi kushinda hapa Tanzania akija na klabu yoyote mara zote akipoteza dhidi ya Simba.
Ibenge ambaye msimu uliopita aliiwezesha RS Berkane ya Morocco kushinda Kombe la Shirikisho Afrika ,aliongeza kuwa staa mwingine ambaye anamuumiza kichwa ni staa wao mpya Stephane Azizi Ki ambaye aliwahi kujaribu kutaka kumsajili lakini hesabu zikagoma.
“Pia wana Azizi Ki ni mchezaji mzuri ambaye wanaweza kuwa na safu bora ya ushambuliaji, niliangalia mechi yao dhidi ya Simba nikaona jinsi wanavyohaha na Fiston.
“Niliona pia mechi hiyo wamemrudisha kucheza beki ya kati Yannick Bangala nimewahi kuwa naye na akicheza hapo anakuwa ni mtu imara zaidi,utaona jinsi walivyo na kikosi bora.
“Tunatakiwa kujipanga sawasawa itakuwa mechi ngumu hasa watakapokuwa nyumbani,hii ni klabu ambayo Ina mashabiki wengi ambao wanaweza kujaa uwanjani,kama tukikutana nao itakuwa mechi ngumu.
“Kwasasa tunaendelea kujipanga kwanza kukabiliana na St George,tunaamini hizi mechi tutakazocheza hapa katika haya Mashindano mafupi yatatupa ubora kwa kuwa ligi hapa bado haijaanza,” alisema kocha huyo wa zamani wa AS Vita ya DR Congo aliyewahi kuhusishwa na kuzinoa Simba na Yanga miaka ya hivikaribuni.