SIMBA imevuka bahari kwenda Zanzibar kwa ajili ya mechi za kirafiki dhidi ya Kipanga na Malindi zilizopo Ligi Kuu Zanzibar (ZPL), huku ikipewa ujanja wa kufanya vyema kwenye mechi zao zijazo za raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika itakapovaana na Primiesro de Agosto ya Angola.
Aliyewapa mchongo huo ni winga wa zamani wa kimataifa wa Tanzania aliyewahi kukipiga katika Ligi Kuu ya Angola, Said Maulid ‘SMG’ aliyesema ni lazima Simba ijiandae mapema hasa kwa mechi yao ya ugenini kwani aikishatoboa hapo, haitakuwa na kizuizi cha kuipeleka hatua ya makundi ya CAF.
SMG aliyewahi kukipiga Simba na Yanga kabla ya kwenda Angola kuichezea Onze Bravos kati ya mwaka 2008-2012 alifichua maufundi ya de Agosto, akiweka wazi kama watajipanga vizuri watashinda na kusonga mbele kirahisi tu.
“De Agosto ni timu ya jeshi ambayo kwa Angola ni kubwa kama ilivyo Simba au Yanga kwa maana ya ubabe, rekodi, makombe, mashabiki na hata kihistoria, hivyo ni lazima wawakilishi wa Tanzania waende kwa akili na tahadhari kubwa ili kupata matokeo mazuri ugenini,” alisema SMG na kuongeza;
“Mbali na de Agosto nyingine inayowika ni Atletico Petroleos de Luanda zenye mashabiki wengi na pia uwekezaji wao ni mkubwa, ila kwa ishu za uwanjani Simba ina timu imara, lakini Agosto wako vizuri, miaka ya hivi karibuni iliyumba kutokana na Uviko-19 na msimu huu imerejea kwa kasi.”
SMG alisema hata hivyo kurejea kwa kasi kwa de Agosto hakuwezi kuifanya Simba ishindwe kufanya yao ugenini na hata mechi ya nyumbani, kwani ina wachezaji wenye uwezo ambao wanapaswa kucheza kwa umakini kwenye mechi zote na kuepuka makosa yatakayoigharimu kwa Waangola.
“Muhimu wafanye mapema maandalizi kabla ya kwenda huko, pia ijiandae kwa lolote kwani ni timu yenye uzoefu na zenye fitina nyingi nje ya uwanja, hasa inapokuwa inakabiliwa na mechi ngumu,” alisema SMG, nyota wa zamani wa Taifa Stars aliyesifika enzi zake kwa kasi kama kiberenge.
Simba ilipenya hatua hiyo kwa kuing’oa Nyasa Big Bullets ya Malawi kwa jumla ya mabao 4-0 katika mechi ya raundi ya awali, huku de Agosto iliitoa Red Arrows ya Zambia. Mabosi wa Msimbazi waliweka bayana mapema kabla ya kuanza na msimu kwamba kiu yao safari hii ni timu hiyo kufika nusu fainali baada ya misimu minne iliyopita ya CAF.