KLABU ya Simba imetangaza kaulimbiu mpya ya operesheni Septemba, ili kutekeleza mambo matatu ambayo wanatarajia kuyafanya mwezi huu, ikicheza mechi tatu za Ligi Kuu na mbili za Ligi ya Mabingwa Afrika.
Meneja Habari na Mawasiliano wa klabu hiyo, Ahmed Ally, amesema wana mambo makubwa matatu ambayo watatakiwa kuyatekeleza kwa usahihi, hivyo wamekuja na kaulimbiu hiyo.
"Mwezi huu tuna kitu kinaitwa 'Operesheni Septemba', ambapo tunataka kutekeleza mambo matatu kwa usahihi, kwanza ni kushinda mechi yetu ya Jumatano (kesho) dhidi ya KMC FC, kwa sababu tukifanya hivyo tutakuwa tumevuna pointi tatu na kufikisha tisa ambazo tulikuwa tunazihitaji kabla ya kwenda kucheza mechi za kimataifa.
Pili tuna operesheni nyingine ya kwenda kushinda mechi zetu Nyanda za Juu Kusini kwa sababu msimu uliopita hatukupata pointi yoyote dhidi ya timu za huko tukiwa Mbeya dhidi ya Prisons na Mbeya City, na ya tatu ni operesheni ya kwenda kushinda Malawi dhidi ya Nyasa Big Bullets, Septemba 10 na ya marudiano terehe 17. Mambo haya yote matatu makubwa mwezi huu, tumeamua kuja na kitu kinaitwa Operesheni Septemba kwani mechi hizo zote tano tutazicheza ndani ya mwezi huu," alisema Ahmed.
Baada ya mechi ya kesho ya Ligi Kuu dhidi ya KMC, Simba itakwenda kucheza mechi ya Ligi ya Mabingwa nchini Malawi na Septemba 14 itacheza dhidi ya Prisons kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya, kabla ya kurudiana na Nyasa Big Bullets Septemba 17 na tarehe 28 mwezi huu itacheza dhidi ya Mbeya City kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.
Kikosi cha timu hiyo kiliingia kambini jana kwa ajili ya kujiandaa na mechi hizo, huku klabu hiyo ikimwita pia beki wake wa kati Joash Onyango anayedaiwa hana furaha kutokana na kutokuwa kwenye kikosi cha kwanza