Spika aibana Serikali kutopelekwa michango ya wafanyakazi



Dodoma. Serikali imesema changamoto ya muda mrefu ya baadhi ya waajiri kutopeleka michango ya wafanyakazi katika mifuko ya hifadhi ya jamii itapata ufumbuzi baada ya miezi mitatu.

Dk Tulia ameihoji Serikali katika kipindi cha maswali na majibu leo Ijumaa Septemba 23, 2022 “ni kazi ya nani kuhakikisha michango inayokatwa inapelekwa katika mifuko ya hifadhi ya jamii.”

Akijibu swali hilo, Naibu Waziri katika Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu, Patrobas Katambi amesema kwa mujibu wa Sheria ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ni wajibu wa mwajiri kupeleka michango ya wafanyakazi na mifuko ya hifadhi ya jamii kufuatilia.

“Kwa sasa kumeshachukuliwa utaratibu wa kufungua akaunti ya kimtandao ya moja kwa moja kila mwanachama anapewa taarifa yake kupitia simu ya kiganjani kwa hiyo kama michango haiendi tunawakamata,”amesema.


Katambi amesema wanaendelea na operesheni kuhakikisha takwa hilo la kisheria linatekelezwa ili wastaafu wasisumbuliwe.

Baada ya majibu hayo wabunge walisimama wakitaka kuuliza maswali ya nyongeza, lakini Dk Tulia alisema anawaona wabunge hao lakini anataka kwenda na jambo hilo vizuri.

“Na tukisema tunaliacha liendelee mtu anafuatilia mafao miaka miwili, anaambiwa michango yako haikuja. Kama ni kazi ya mwajiri kupeleka na mfuko unajua kuwa mwajiri hajapeleka ni kazi yao mfuko umlipe huyu (mstaafu) mafao yake.


"Wao waende wakatafute fedha zilipo kwasababu kazi yangu kama mwajiriwa kuanza kusema kama fedha zilikuja ama hazikuja. Halafu kama mwajiri hakupeka mimi (mwajiriwa) naweza kumuadhibu?”amehoji.

Amesema wananchi hawatakiwi kuteseka baada ya mwajiri kukata fedha hizo na kuitaka Serikali kutengeneza utaratibu mzuri wa kusimamia mifuko hiyo na kuwalipa wastaafu.

Baada ya hapo, Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Profesa Joyce Ndalichako amesema Serikali tayari imeliona suala hilo na wanafanyia kazi ili kupata ufumbuzi kwa waajiri wasiopeleka michango ya waajiriwa.

“Yako madeni yanafika miaka 10, bado hajaleta hizo fedha. Kwa hiyo nilihakikishie Bunge lako tayari Serikali inafanyia kazi na niahidi ndani ya miezi miwili, mitatu tutakuja na muafaka wa kulitatua hili ambalo ni la muda mrefu,”amesema.



Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad