TCRA yaitoza faini Sh2 milioni Zama Mpya TV Online




Dar es Salaam. Kamati ya Maudhui ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), imetoa hukumu kwa chombo cha habari Zama Mpya TV Online ya kulipa faini Sh2 milioni, onyo na kuwekwa chini ya uangalizi kwa miezi mitatu kwa kosa la kuchapisha maudhui ya kuleta uchochezi.

Akisoma hukumu hiyo leo Ijumaa, Septemba 9, 2022, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Habi Gunze amesema Zama Mpya TV Online kupitia mtandao wa kijamii wa Twitter Agosti 28, 2022 walichapisha maudhui yaliyotamkwa na msanii Seleman Msindi maarufu Afande Sele ambayo yalikuwa ya uchochezi.

“Taarifa hiyo ilidai kuwa viongozi wamekosa ubunifu na kwamba ni maneno tu na hawaoni miradi ikiiisha, na kudai hayo ni matokeo ya kuambiwa wale kwa urefu wa kamba zao,” alisema Gunze na kuongeza akinukuu;

“Tozo zimekuwa nyingi lakini watu hawaoni zinafanya kazi gani, hawaoni miradi ikiisha ni maneno tu mfano SGR, bwawa la umeme watu wanachukizwa na tozo kwasababu viongozi wamekosa ubunifu na ile kauli ya kuambiwa wale kwa urefu wa Kamba zao,” 


Gunze amesema uchapishaji huo unakiuka sheria na kanuni na maadili ya utangazaji huku akizitaja kanuni hizo kuwa ni 9(a) 12 (a) (i) na 16 (1) na aya ya 3 (j) (d) (g) (h) na (k) ya jedwali la tatu katika kanuni ya Mawasiliano ya Kieletroniki na Posta.

Gunze ameongeza uongozi wa chombo hicho uliitwa kwa ajili ya kujieleza kwanini hatua za kisheria zisichukuliwe juu yao na walitoa sababu za utetezi ikiwemo kuhoji chanzo cha taarifa ni Afande Sele ila hayupo katika mashtaka ili aelezee maneno aliyotamka.

Kamati hiyo imesema imeridhika Zama Mpya imekosa umakini katika uchapishaji wa maudhui yao na kutokana na hayo wanatakiwa kuwajibika katika maudhui yao.

Gunze amesema baada ya kupokea utetezi wa Zama Mpya kamati imejiridhisha wamekiuka kanuni ya Mawasiliano ya Kieletroniki na Posta, Utangazaji wa maudhui mtandaoni 2020 iliyofanyiwa marekebisho 2022.

“Kamati ya Maudhui inatoa adhabu kama ifuatavyo, kwanza inatoa onyo, mbili Zama Mpya inaamriwa kulipa faini Sh2 milioni ndani ya siku 21 na tatu inawekwa chini ya uangalizi wa TCRA miezi mitatu na ndani ya kipindi hicho inatakiwa kuboresha utendaji kazi wake na mfumo wa usimamizi kuzingatia sharia, kanuni na maadili ya uandishi wa habari,” amesema 
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad