Kamati ya rufaa ya Shirikisho la Mpira wa Miguu TFF leo limetangaza maamuzi ya kamati hiyo kuhusiana na hukumu ya Haji Manara ya kufungiwa miaka miwili kujihusisha na soka pamoja na faini ya Tsh milioni 20.
Mwenyekiti wa kamati ya rufaa ya Maadili ya TFF Richard Mbaruku amesema wamepitia rufaa ya Haji Manara na kuona kuwa inakosa mashiko ila wametumia busara ya kumpunguzia adhabu na sasa atatumikia adhabu yake ya miaka miwili na faini ya Tsh milioni 10 kutoka Tsh milioni 20 iliyokuwa awali.
“Tumeona mrufani atatumikia adhabu yake kwa miaka miwili na kulipa faini ya Tsh milioni 10 badala ya milioni 20 hii ni kutokana na busara ya kamati ya rufaa”>>> Richard Mbaruku
Kama utakuwa unakumbuka vizuri July 21 2022 Haji Manara alitangazwa kufungiwa miaka miwili kujihusisha na soka pamoja na faini ya Tsh milioni 20 baada ya kukutwa na hatia ya kumkosea nidhamu Rais wa TFF Wallace Karia wakati wa mchezo wa fainali ya ASFC kati ya Yanga na Coastal Union katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha July 2 2022.