KAMATI ya Sheria na hadhi za Wachezaji inakutana Ijumaa kujadili mashauri yaliyowasilishwa kwenye kamati yao sakata la Tuisila Kisinda wa Yanga likitajwa kuwemo.
Kisinda amesajiliwa dakika za mwisho na mamlaka za soka zimeweka wazi kwamba hatacheza kwenye dirisha hili kutokana na usajili wake kuchelewa kwa mujibu wa kanuni ya 62 (1) ya ligi kuu toleo la 2022.
Akizungumza na Mwanaspoti, Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Said Soud alisema ni utaratibu wao kukutana mara baada ya usajili wote kukamilika ili kupitia pingamizi zilizopo baada ya usajili.
“Hatuna kawaida kuzungumza mapingamizi kabla ya kupitia lakini kikao kipo na tutajadili masuala ya usajili wala sio mambo ya madai hivyo suala la Kisinda na Joash Onyango linahusiana usajili litafanyiwa kazi,” alisema.
“Dosari kwenye suala la usajili huwa hazikosekani,” alisema.
Inaelezwa Onyango amepeleka barua Shirikisho la soka Tanzania (TFF), kuomba kusitishiwa mkataba wake wa miaka miwili aliyosaini na Simba kabla ya msimu huu kuanza miongoni mwa sababu alizoeleza ni kushindwa kutimiziwa mahitaji yake na ana mpango wa kutimkia Singida Big Stars.
MSIKIE NABI
Kisinda ameshatua nchini kimyakimya kujiunga na klabu yake ya Yanga huku mabosi wake wakiendelea kupigania nafasi yake kwenye usajili lakini kocha wao Nasreddine Nabi humwelezi kitu amemuita haraka kambini.
Nabi alipoulizwa kwanini fasta hivyo akasema; “Namuachaje Kisinda? Bonge la mchezaji.”
Staa huyo ameweasili nchini usiku juzi huku akigoma kuongea chochote lakini Mwanaspoti likajulishwa juu ya Nabi kumtaka haraka kambini jana mchana na usiku alikuwa uwanjani akiangalia mechi dhidi ya Azam.
“Usizungumzie mechi hizo zinazokuja, hata huu mchezo wa Azam kama angekuwa sawa ningempa nafasi acheze,sisi makocha ndio tunamtaka Kisinda kwa ajili ya hesabu zetu,”alisema Nabi ambaye anataka timu yenye mbio.
“Nimemuita aje tuongee nijue alivyojiandaa kuelekea msimu huu hayo mambo ya hatma yake viongozi wangu watafuatilia hata kama hatacheza mechi ya Azam lakini ni vyema akawa katika maandalizi na wenzake ili atakapokuwa sawa tumpe nafasi,”alisema Nabi na kuongeza kuwa anaamini kama viongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na Yanga watamalizana vizuri hatua hiyo itaipa nguvu kubwa timu yake kuelekea mechi za Kimataifa.
“Naamini yatakuja maamuzi ambayo sote tunayatarajia kwa manufaa ya soka la nchi hii na Yanga, Kisinda ni mchezaji ambaye tunamuhitaji makocha ili atuongezee nguvu hili ni vyema likafahamika.”