William Samoei Ruto amethibitishwa na Mahakama ya upeo nchini Kenya kuwa mshindi halali wa uchaguzi mkuu wa Agosti 9, 2022 na siku chache zijazo anakwenda kuapishwa na kuwa rais wa tano wa Kenya.
Ni mara ya kwanza kwa Ruto kuwania urais, ambapo kabla alikuwa naibu wa rais Uhuru Kenyatta katika uchaguzi wa mwaka 2013 na 2017i.
Amemuangusha Raila Odinga, mtoto wa makamu wa rais wa kwanza wa Kenya, Jaramogi Oginga Odinga kwa kupata asilimia 50.4% dhidi ya asilimia 48.8% alizopata Odinga kwa mujibu wa Tume ya uchaguzi nchini humo (IEBC).
Odinga
Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha,
Odinga (kushoto) akiwa na Kalonso Musyoka wa chama cha Wiper
Odinga, mwanasiasa mkonge na mpinzani wa muda mrefu alikuwa anaungwa mkono na Rais anayemaliza muda wake, Uhuru Kenyatta ambaye pia ni mtoto wa rais wa kwanza wa taifa hilo, hayati Mzee Jomo Kenyatta.
Lakini hili si jaribio la kwanza la kuutaka urais kwa Bwana Odinga anayetajwa kama baba wa demokrasia kwenye taifa hilo. Akiwa na miaka 77 sasa hii ilikuwa mara ya 5 sasa na mara zote ameangushwa, kama ilivyokuwa kwa baba yake, Jaramogi Oginga Odinga, ambaye pamoja na juhudi kubwa alizofanya dhidi ya ukoloni wa waingereza, lakini hakufanikiwa kuwa rais.
Ingawa awali alisema uchaguzi wa mwaka huu 2022 litakuwa jaribio la mwisho kwake, lakini baada ya Mahakama kuthibitisha ushindi wa Ruto aliandika katika mtandao wake wa twitter kwamba anaheshimu uamuzi wa Mahakama lakini hakubaliani nao.
Lakini Odinga si kiongozi pekee Afrika aliyejaribu mara kadhaa kutaka urais, wapo wengi na miongoni mwao ni hawa;
5: Étienne Tshisekedi wa Mulumba
Mulumba
Chanzo cha picha, Getty Images
Étienne Tshisekedi, ambaye jina lake kamili Étienne Tshisekedi wa Mulumba, alizaliwa Desemba 14, 1932, huko Luluabourg, Belgian Congo sasa inaitwa Kananga, Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Kwa DRC huyu ana heshima ya kuwa baba wa demokrasia akiwa Mkongo wa kwanza kuanzisha chama cha upinzani (UDPS), na kupambana na marais Mobutu Sese Seko, Laurent Kabila na Joseph Kabila.
Alikuwa mmoja wa wanasiasa wa upinzani wachache waliothubutu kukabiliana na Mobutu aliyekuwa akionekana kama 'dikteta'.
Étienne Tshisekedi ndiye mwanasiasa wa upinzani wa muda mrefu zaidi DRC na mpaka alipofariki Februari 1, 2017 alishindwa majaribio kadhaa ya urais ukiwemo uchaguzi wa mwaka 2011, ambao alionekana kuwa karibu kushinda.
Ule wa mwaka 2006 aliususia kutokana na udanganyifu kwenye mfumo wa uchaguzi.
Aliwahi kupewa Uwaziri mkuu kwa vipindi vitatu DRC wakati huo ikiitwa Zaire: 1991, 1992–1993, and 1997.
Kama ilivyo kwa Uhuru Kenyatta kuupata urais wa Kenya, akifuata nyayo za baba yake Jomo Kenyatta, na tofauti na familia ya Odinga, ambayo si baba Jaramogi Oginga Odinga wala mtoto Raila Odinga aliyekuwa rais mtoto wa Étienne Tshisekedi, Félix Tshisekedi ndiye rais wa sasa wa DRC, akiingia madarakani mwaka wa 2019.
4: Morgan Tsvangirai
Morgan
Chanzo cha picha, Getty Images
Kama kuna mwanasiasa Zimbabwe aliyethubutu 'kumsumbua' kisiasa Mwanasiasa aliyekaa madarakani kwa muda mrefu, Robert Mugabe basi ni Morgan Tsvangirai.
Uchaguzi wa 2002 alipata asilimia 42% ya kura dhidi ya 55.2% za Mugabe aliyekuwa anapeperusha bendera ya chama cha ZANU-PF na kutengeneza nguvu kubwa ya upinzani kupitia chama chake cha MDC.
Tsvangirai alikaribia kushinda urais katika uchaguzi wa mwaka 2008 alipopata asilimia 47.9% ya kura dhidi ya 43.2% za Mugabe, ambazo zilipelekea kuwepo kwa uchaguzi wa marudio uliofanyika Juni 27, 2008.
Hata hivyo Tsvangirai alisema alishinda uchaguzi huo kwa asilimia kubwa ambazo hukupaswa kuwepo kwa marejeo. Kukazuka ghasia kubwa na baadaye aliamua kujitoa Juni 22, 2008, wiki moja kabla ya siku ya kupiga kura. Mugabe akaenda kushinda kwa zaidi ya asilimia 90%.
Uchaguzi wa 2013 alipata asilimia 34.3% dhidi ya 61.8% za Mugabe, Tsvangirai alikataa matokeo na katika kusaidia kuleta utulivu, iliundwa Serikali ya Umoja wa kitaifa akawa Waziri mkuu chini ya utawala wa Mugabe kati ya mwaka 2009 -2013.
3: Profesa Ibrahim Lipumba
Lipumba
Chanzo cha picha, Getty Images
Professor Ibrahim Lipumba ni mchumi na mmoja wa wanasiasa wa upinzani wa muda mrefu nchini Tanzania, akikiongza chama cha CUF tangu mwaka 1995, kabla ya kutofautiana na katibu wake Mkuu, Maalim Seif mwaka 2015 alipojiuzulu lakini akarejea tena kwenye nafasi hiyo anayoishika mpaka sasa.
Amewania urais mara nne, tangu mfumo wa vyama vingi uanze Tanzania katika miaka ya 1990 na mara mbili alishika nafasi ya pili.
Katika uchaguzi mkuu wa 1995, alikuwa wa tatu, Uchaguzi wa 2000 alishika nafasi ya pili nyuma ya Hayati Benjamin Mkapa wa CCM aliyekuwa madarakani.
Akajitosa tena katika uchaguzi wa 2005, na kushika nafasi ya pili kwa kupata asilimia 11.68% ya kura nyuma ya Jakaya Kikwete. Uchaguzi wa 2010 akashika nafasi ya 3 nyuma ya Kikwete tena akipata asilimia 8.3% ya kura.
Umaarufu wake umetetereka katika miaka ya hivi karibuni, na kukomaa kwa chama kingine cha upinzani cha CHADEMA na ACT- Wazalendo, kumezidi kumuweka mbali na harakati za urais.
Mwaka 2015 alikuwa sehemu ya wanasiasa na vyama vilivyounda UKAWA umoja uliomsimamisha waziri mkuu wa zamani, Edward Lowassa kuwania urais dhidi ya John Magufuli.
Ametangaza chama chake hakitashiriki uchaguzi mkuu kwa sababu ya kutoridhishwa na mwendendo wa uchaguzi wa mwaka 2020 uliompa ushindi hayati Magufuli wa CCM.
2: Kizza Besigye
Kizza
Chanzo cha picha, Getty Images
Warren Kizza Besigye Kifefe , aliyezaliwa Aprili 22, 1956), anafahamika kama Kanali Dk. Kizza Besigye na ni mwanasiasa na afisa wa zamani wa Jeshi la Uganda (UPDF) .
Akiwa kiongozi wa chama cha upinzani cha FDC amejaribu kuwania urais mara nne bila mafanikio katika uchaguzi wa mwaka 2001, 2006, 2011, na 2016 na mara zote akiangushwa na Yoweri Museveni ambaye amekuwa rais wa Uganda tangu Januari 26, 1986.
Ni mmoja wa wanasiasa wa upinzani waliokumbana na 'kasheshe' nyingi kutoka utawala wa Yoweri Museveni mwenye miaka umri wa 77.
Japokuwa katika uchaguzi uliopita wa Januari, 2021 hakuwania urais, alimuunga mkono Bobi Wine ambaye aliangushwa pia na Museveni aliyekuwa anawania urais kwa mara ya 6 na anayekwenda kutawala Uganda kwa miaka 40.
1. Seif Sharif Hamad - Zanzibar
Maalim Seif
Chanzo cha picha, Getty Images
Baada ya kuwa Waziri kiongozi wa serikali ya mapinduzi ya Zanzibar kwa miaka 4 na kushika nafasi mbalimbali katika utawala wa CCM, baada ya kuingia kwa mfumo wa vyama vingi nchini Tanzania, Maalim aliondoka na baadhi ya wana CCM na kwenda kuanzisha chama cha CUF na kuwania urais wa Zanzibar mwaka 1995.
Akashindwa na Mgombea wa CCM, Salmin Amour aliyeshinda kwa asilimia 49.76% dhidi ya 50.24% za Maalim. CUF ilikataa matokeo.
Akawania tena urais wa visiwa hivyo mwaka 2000 akabwagwa na Amani Karume, kukatokea ghasia zilizopelekea vifo vya watu kadhaa.
Akajaribu tena mwaka 2005 akabwagwa na Karume na mara ya tano akajitosa mwaka 2010 dhidi ya Dr Shein akashindwa. Mwaka 2015 uchaguzi ulifutwa na mwenyekiti wa tume ya Uchaguzi Zanzibar, Salim Jecha kwa sababu ya kujaa kasoro katika wakati ambao upande wa maalim Seif ulidai kushinda wazi.
Na uliporudiwa mwezi Machi 2016, Maalim Seif aligoma kushiriki tena uchaguzi na kumfanya Dr Shein kuendelea kushika kiti cha urais.
Mwaka 2020 alishiriki kwa mara ya 6 dhidi ya Hussein Mwinyi na akashindwa tena.
Japo mara zote amegoma kukubali matokeo, lakini kwa katiba ya Zanzibar, alipata nafasi ya kuwa makamu wa rais wa kwanza wa visiwa hivyo na mpaka alipofariki Februari 17, 2017 alikuwa kwenye nafasi hiyo.