STENDI YA MAGUFULI
WATUMIAJI wa usafiri wa mabasi yanayofika Dar es Salaam kutoka mikoani wamelalamikia hatua ya abiria wote kulazimishwa kushuka katika kituo cha mabasi cha Magufuli na kuzuia mabasi kupakia abiria kwenye ofisi za mabasi husika nje ya kituo.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Innocent Bashungwa amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla akutane na wadau wa usafirishaji wa mabasi ili kulipatia ufumbuzi tatizo hilo.
Alisema Stendi ya Magufuli iliyoigharimu serikali Sh bilioni 50 ilijengwa kukabili changamoto ya ufinyu katika stendi ya Ubungo hivyo ni vyema ikawekewa utaratibu wenye tija kwa serikali, wasafirishaji na abiria.
Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (TABOA) kimedai kutofurahishwa na hatua hiyo kwa kuwa haikuzingatia utaratibu ambao ungesaidia kuondoa usumbufu kwa abiria na wenye mabasi.
Chama cha Watetezi wa Abiria Tanzania (CHAKUA) kupitia kwa Mwenyekiti wake, Hassan Mchanjama kimesema utaratibu wa abiria kutumia kituo cha Magufuli upo kisheria hivyo wasafiri wanachopaswa ni kuufuata kama ulivyo.