Dar es Salaam. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), George Simbachawene amemtaka Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba kuwa na jukwaa maalumu kwa ajili ya kutoa ufafanuzi juu ya mambo yanayojadiliwa mtandaoni.
Simbachawene ameyasema hayo leo Alhamisi Septemba Mosi, 2022 jijini Dodoma wakati akitoa ufafanuzi kuhusu tozo za miamala ambazo zimekuwa zikilalamikiwa na wadau mbalimbali wakiwemo wananchi wa kawaida kila kona.
Amesema baadhi ya watu wamekuwa wakijipa kazi ya kukosoa kila kinachofanywa na Serikali na mara nyingi wanapotosha umma, hivyo amemwomba Dk Mwigulu kuwa na jukwaa kama hilo mara kwa mara ili kutoa ufafanuzi wa kile kinachopotoshwa.
“Huko mitaani siku hizi, mtu akikaa na simu yake anajifanya naye ni mchumi, anaelezea masuala ya nchi hii utadhani yeye ndiyo anayajua sana, kwa hiyo upotoshaji ni mwingi sana.
“Tunadhani forum (jukwaa) kama hizi ni vizuri zikaendelea…waziri wa fedha yupo, ndiye anayeshika sera ya fedha na uchumi wa nchi, yeye tu, ndiye aliyeapishwa na kazi yake ndiyo hiyo mpaka pale itakavyokuwa vinginevyo.”
“Nadhani mheshimiwa waziri iko haja ufikiri kuwa na forum kama hizi kila baada ya muda fulani. Unazungumza nao ili wale wapotoshaji wa kule mtaani wasipate nafasi. Katika dunia ya leo hakuna kunyamaza, ukiambiwa jambo, jibu, usipojibu, yule anayesema mara nyingi anaonekana anasema ukweli,” amesema Simbachawene.
Waziri Simbachawene amebainisha hayo ikiwa ni siku kadhaa baada ya vyombo vya habari kumtafuta Dk Mwigulu kufafanua hoja za wadau kuhusu tozo hizo, hata hivyo waziri huyo amekuwa siyo mwepesi kupatikana kutoa ufafanuzi kuhusu suala hilo.