Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu Ummymwalimu leo akiwa Dodoma amekutana na Waandishi wa Habari kutolea ufafanuzi kuhusu huduma za Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) ambapo amesema “Pamoja na uwepo wa ongezeko kubwa la magonjwa yasiyo ya kuambukiza, sababu nyingine inayohatarisha uhai na uendelevu wa mfuko huu ni vitendo vya udanganyifu vinavyofanywa na baadhi ya Watoa huduma na Wanachama wa mfuko, vitendo hivi vinalenga kujipatia manufaa kinyume na utaratibu”
“Mathalani katika mwaka wa fedha 2021/22 jumla ya Wataalamu 65 wamefikishwa katika Mabaraza yao kutokana na kukiuka taratibu na miongozo ya taaluma za afya, nimeieleza NHIF kuimarisha mikakati yake ya kupambana na vitendo vya udanganyifu pamoja na kuimarisha matumizi ya Mifumo ya TEHAMA”
“Vilevile, changamoto nyingine iliyopo ni uwepo wa kundi kubwa la Wananchi wanaojiunga na NHIF kwa hiari ambao, takribani asilimia 99 ni Wagonkwa,hatua hii imetokana na kutokuwepo kwa Sheria ya ulazima kwa wananchi kujiunga na Bima ya Afya”
“Kama mnavyokumbuka Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), ulianzishwa mwaka 2001 ukiwa umelenga kuwahudumia watumishi wa umma pekee lakini kutokana na uhitaji wa huduma hizi kwa wananchi wote, marekebisho ya Sheria yamekuwa yakifanyika mara kwa mara na kuruhusu makundi mbalimbali kuhudumiwa na mfuko”