Yanga yalipa CAF Kisinda acheze




SINTOFAHAMU imeibuka sakata la usajili wa Winga Mkongomani, Tuisila Kisinda ndani ya Yanga. Klabu imesisitiza kwamba imefanya kila kitu kwa wakati na mchezaji huyo ni mali yao lakini Shirikisho la Soka la Tanzania(TFF) limesema hapana.

Yanga wamekuwa katika vikao vizito na simu zisizokauka wakipambana kutumia wanasheria kukutana na Kamati ya Leseni pamoja na ile ya Sheria na Hadhi za wachezaji kusaka ufumbuzi wa usajili huo.

Wamesisitiza kwamba kwenye usajili walichomoa jina la majeruhi Lazarous Kambole na kumchomeka Kisinda kwa kumlipia faini Shirikisho la Soka la Afrika (CAF). Iko hivi; Kisinda ambaye yupo Yanga kwa mkopo akitokea Berkane ya Morocco iliyowauzia msimu uliopita baada ya kumalizika msimu wa 2020-2021. Yanga kupitia kwa Mkurugenzi wa Mashindano wa klabu hiyo, Saad Kawemba alisisitiza wameshakamilisha usajili huo kwa kulipa faini kutokana na kuchelewa kupeleka jina la mchezaji lakini wanashangaa kinachoendelea ndani ya TFF.

“Unajua wenyewe tunapata ukakasi kwenye ishu ya mchezaji huyo jina lake kushindwa kupitishwa wakati tayari tulishaomba kuondolewa kwa jina moja la mchezaji wa kigeni kutokana na kusumbuliwa na majeraha ya muda mrefu,” alisema. “Tuliomba jina la Lazarous Kambole liondolewe ili kupisha jina la Kisinda kutokana na mchezaji huyo kuwa na majeruhi ya muda mrefu kwa makubaliano ya kuendelea kumtimizia kila kitu hadi dirisha dogo litakapofunguliwa.


“Tunashangazwa na taarifa ya TFF kwamba sisi tuna wachezaji 13 na tumekiuka kanuni sio kweli kwani tulikuwa na ombi maalumu kwa ajili ya kumtoa mchezaji mmoja na kumuingiza mwingine na tulifanya hilo kwa kuzingatia muda wa usajili.”

KAULI YA TFF

Taarifa iliyotolewa na TFF jana, japokuwa haikutaja timu yoyote, iliandikwa hivi: “kwa mujibu wa kanuni 62 (1) ya Ligi Kuu toleo 2022, klabu inaruhusiwa kusajili wachezaji wa kigeni wasiyozidi 12 hivyo klabu kutaka au kujaribu kusajili zaidi ya idadi hiyo ni kwenda kinyume na kanuni.”

Akizungumza na Mwanaspoti, Katibu Mkuu wa zamani wa TFF, Angetile Osiah alihoji kanuni iliyolizuia shirikisho hilo kubadilisha jina la mchezaji wakati muda wa usajili haujaisha.


Alisema kwa uelewa wake wa sheria na kanuni za usajili hakuna sehemu inayozuia klabu kufanya marekebisho ndani ya wakati huku akiwataka TFF kuacha kutumia utashi binafsi kwenye mambo yaliyopo kwenye kanuni.

Gazeti hili pia lilimtafuta Mwenyekiti wa Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji wa TFF, Alex Mgongolwa, aliyegoma kufafanua kwa madai kwamba ni mmoja wana kamati ya tukio hilo.

MENEJA WA KISINDA

Meneja wa Kisinda, Nestor Mutuale ameliambia Mwanaspoti kwa njia ya simu akiwa DR Congo kwamba amesikiliza sakata hilo na kugundua ni siasa za soka la Tanzania.

Mutuale alisema kitu pekee ambacho kingemzuia Kisinda kuichezea Yanga kwa sasa ni hati yake ya uhamisho wa Kimataifa (ITC) ambayo amelihakikishia Mwanaspoti tayari ipo pale makao makuu ya TFF.


Meneja huyo alikiri kutokana na kanuni za ndani za TFF, Yanga inapaswa kumuondoa mchezaji mmoja ambaye alishaanza kusajiliwa changamoto ambayo inaweza kumalizwa kwa Yanga kukaa mezani na mamlaka hiyo ya soka hapa nchini. “Nimeona hilo sakata lakini naona ni siasa za soka hapo Tanzania, hata wachezaji wangu wamekuwa wakiniambia na nimekuwa nikiona TFF haiko sawa na Yanga iko siku watasababisha matatizo makubwa kwa Tanzania,” alisema.

“Kisinda ingekuwa ngumu sana kucheza Yanga kama ITC ingekuwa haijafika lakini Mimi nina uhakika tayari ipo hapo Tanzania muda mrefu. Hapo mna kanuni zenu za wachezaji wa kigeni wakitakiwa 12 Yanga tayari walishaomba kumuondoa mmoja na wamuingize Kisinda ndio maana unaona ITC yake imefika.

“Hilo tatizo linatakiwa Yanga kukaa pamoja na TFF kuangalia maslahi ya mpira wa Tanzania na sio kuharibu kwa kuzuia mchezaji asicheze,FIFA haina shida ndio maana ikatoa ITC kilichobaki Kisinda kucheza ni mambo yenu ya ndani.

“Nimewahi kuona kitu kama hicho Tanzania na mchezaji akasubiri baada ya siku chache FIFA wakaruhusu atumike, Yanga wakae mezani na TFF wamalize hilo,”alisema

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad