Zoran akuna kichwa Simba, alia ugumu alionao sasa



KIKOSI cha Simba kimerejea jana mazoezini kujiandaa na mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya KMC, huku Kocha mkuu wake, Zoran Maki akikuna kichwa kutokana na kikosi hicho kuwa na ratiba ngumu ndani ya Septemba na kitakuwa na mechi tano na kutakiwa kucheza kila baada ya siku tatu.

Simba ina mechi tatu za Ligi Kuu mbili za ugenini jijini Mbeya na nyingine mbili za kimataifa za Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Nyasa Big Bullets ya Malawi itakayoanza nayo ugenini.

Zoran amesema ugumu wa ratiba yao ilivyo hawana sababu ya kuangalia nyuma zaidi ya kuhakikisha wanacheza vizuri mechi za ligi na kupata matokeo ya ushindi ili kuendelea kubaki kileleni mwa msimamo, lakini bado anahofia itawachosha wachezaji wake.

Alisema baadhi ya timu watakazocheza nazo mwezi huu ni wasumbufu kwa Simba kulingana na matokeo ya mechi za nyuma zikiwamo za msimu uliopita ugenini kiasi cha timu hiyo kushindwa kupata ushindi.


“Kwenye kipindi hiki kulingana na ratiba ilivyo wachezaji wangu watakuwa wakifanya yale mazoezi ya kuweka mwili sawa na masahihisho kulingana na kile kilichotokea katika mchezo uliopita,” alisema Zoran na kuongeza; “Ili kushinda taji la Ligi Kuu kama malengo yetu yalivyo tunahitaji kufanya vizuri na kushinda michezo ya ugenini ikiwemo na zile timu tulizoshindwa kuchukua pointi kwao msimu uliopita. “Kulingana na ratiba ilivyo kucheza mechi kila baada ya siku tatu kutakuwa na mabadiliko ya wachezaji katika kikosi ingawa kuna wengine watacheza mara kwa mara kulingana na mechi ambavyo zitakuwa.”

Zoran alisisitiza; “Katika mashindano ya CAF, tunahitaji kufanya vizuri na kushinda mchezo ugenini ili kupunguza presha kwenye mechi ya nyumbani na kupata matokeo bora ili kusonga hatua inayofuata.”

Katika hatua nyingine Zoran alisema Ligi ya mabingwa Afrika ili uwe na uhakika wa kufanya vizuri hatua yoyote ile lazima timu iwe na uwezo wa kupata matokeo bora ugenini.

“Hilo ndio tumelipanga kwa upande wetu mbali ya ugumu wa ratiba uliyokuwepo tunahitaji kuwa na sifa ya kufanya vizuri ugenini kama inavyokuaga nyumbani,” alisema Zoran.

Simba mara itakapomalizana na KMC keshokutwa Jumatano ndani ya siku tatu itasafiri kwenda Malawi kucheza na Nyasa katika Ligi ya Mabingwa Afrika Septemba 10 kisha siku nne baadae itatakiwa Mbeya kucheza na Tanzania Prisons Septemba 14.

Baada ya hapo itarudi Dar es Salaam kurudiana na Nyasa Septemba 17, kisha kusafiri tena kurudi Mbeya kuivaa Mbeya City mchezo utakaochezwa Septemba 28.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad