Dar es Salaam. Abbas Mtemvu ameidharau amri ya Kituo Jumuishi cha Mahakama cha utoaji Haki za Kifamilia yaani ndoa, talaka na mirathi iliyoweka zuio la muda la kuondolewa kwa Ibrahim Mtemvu na Jasmine Mtemvu kwenye nyumba iliyopo kitalu namba 1036/2 eneo la Haile Selas, Masaki kwa kuendelea kuwafukuza ndugu hao.
Wakili wa ndugu hao, Adili Kiiza alisema baada ya wateja wake kufukuzwa kwenye nyumba hiyo Oktoba 7, walienda kufungua shauri dogo mbele ya Hakimu Simon Swai kumtaka Abbas ajieleze kwa nini asifungwe kwa kuendelea kudharau amri ya mahakama iliyopanga kusikiliza kesi hiyo Oktoba 17.
Hata hivyo, alipotafutwa Abbas ambaye ni mbunge wa zamani kujua kama taarifa hiyo ameipata, alisema hawezi kujibu chochote.
“Mwananchi nalifungulia mashtaka kwa kuwa mmekuwa mkinichafua na mnatumika kupitia hao ndugu zangu,” alisema Abbas.
Ibrahim alisema mahakama ilitoa zuio kwa waleta maombi na wanufaika na mirathi kutotolewa kwenye nyumba hiyo lakini ndugu yao Abbas amekuwa akiwatumia mabaunsa kuwazuia wasiingie ndani hivyo kukiuka agizo la lililotolewa na mahakama hiyo.
Oktoba 4, mahakama ilitoa zuio la muda ili kwa Abass kuwaondoa ndugu zake kwenye nyumba ya marehemu mama yao mzazi, Sitti Kilungo hadi shauri la mirathi litakapotolewa uamuzi.
Katika kesi hiyo, Abbas anadaiwa kuiuza nyumba hiyo ya familia kwa Mustafa Mohamed, mkurugenzi wa kampuni ya Delligent Group kwa Sh900 milioni na fedha zote akazitumia peke yake.
Jasmine alisema walipofika nyumbani baada ya kutoka mahakamani Oktoba 5 kusikiliza shauri lao walikuta imewekewa uzio wa mabati huku mabaunsa wanaoilinda wakiwazuia kuingia ndani na “mpaka leo tunalala nje.”
Mwananchi