Ahmed Ally "Siamini Kama Yanga Wamechomoka"

 


Meneja wa Habari na Mawasilino wa Simba SC Ahmed Ally amesema haamini kama kweli Young Africans imeambulia sare ya 1-1 kwenye mchezo wa jana Jumapili (Oktoba 23).


Miamba hiyo ilikutana Uwanja wa Benjamin Mkapa kwa ajili ya kuzisaka alama tatu za Ligi Kuu Tanzania Bara, lakini ilishindwa kutambiana kufuatia kutoshana nguvu kwa mabao yaliyofungwa na Viungo Washambuliaji Augustine Okrah (Simba SC) na Stephen Aziz Ki (Young Africans).


Akizungumza na Dar24 Media baada ya mchezo huo, Ahmed Ally amesema ilikua kama bahati kwa Young Africans kuchomoka kwenye mchezo huo, kwani Simba SC ilidhamiria kuondoka na alama zote tatu, lakini haikuwa hivyo.


“Hadi sasa tunazungumza binafsi siamini kama tumetoka nao sare wale jamaa, ninawashauri wakafanye sherehe kwa hiki walichobahatika kukipata, ninaamini kabisa leo (Jana) ilikua ndio siku yao ya kulia na kusaga meno,”


“Tulijipanga kuondoka na alama zote leo (Jana), lakini imekua bahati tu, imejidhihirisha Simba SC ni timu ya aina gani kwa sababu imecheza soka ambalo limeonyesha hawa wenzetu hawakua na cha kufanya zaidi ya kuzuza uwanjani tu.” amesema Ahmed Ally


Sare ya 1-1 imeendelea kuipa nafasi Simba SC kuongoza msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa kufikisha alama 14 sawa na Young Africans, iliyozidiwa mabao ya kufunga na kufungwa.


Mchezo unaofuata Simba SC itacheza dhidi ya Azam FC Alhamis (Oktoba 27), huku Young Africans ikiikaribisha KMC FC Uwanja wa Benjamin Mkapa siku ya Jumatano (Oktoba 26).

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad