Klabu ya Young Africans imeshukuru kwa kupata alama moja mbele ya watani zo Simba SC baada ya kulazimisha sare ya 1-1 jana Jumapili (Oktoba 23).
Young African iliyokua mwenyeji wa mchezo huo ililazimika kusawazisha bao kupitia kwa kiungo Mshambuliaji kutoka Burkina Faso Stephen Aziz Ki, sekunde chache kabla ya mapumziko baada ya kutanguliwa kufungwa na watani zao Simba SC, kupitia kwa Augustine Okrah.
Afisa Habari wa Young Africans Ally Kamwe amezungumza na Dar24 Media katika mahojiano maalum na kueleza namna wanavyoshukuru kupata alama moja, huku akikiri wanaithamini na kuijali.
Kamwe amesema alama moja walioipata jana Jumapili (Oktoba 23) imewaongeza hali ya kujiamini kuelekea mchezo ujao wa Ligi Kuu dhidi ya KMC FC pamoja na Mchezo wa Mtoano wa Kombe la Shirikisho dhidi ya Club Africain ya Tunisia.
“Tumefarijika sana kwa kupata alama moja mbele ya Simba SC, imetupa thamani kubwa kuelekea mchezo wetu unaokuja wa Ligi Kuu, vilevile kuelekea Mchezo wetu wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Club Africain,”
“Tulijiandaa kwa ajili ya kushinda mchezo huu, lakini bahati haikuwa kwetu, tunaamini wenzetu nao walijiandaa ndio maana wameambulia matokeo ya sare, bado ninasisitiza matokeo haya ni mazuri kwetu yanendelea kutupa nafasi ya kutembea kibabe, kwani hadi sasa hatujapoteza mchezo tangu msimu uliopita.” amesema Ally Kamwe
Sare ya 1-1 imeendelea kuiweka Young Africans kwenye nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwakufikisha alama 14, sawa na Simba SC inayoongoza kwa kuwa na uwiyano mzuri wa mabao ya kufunga na kufungwa.
Young Africans itaikaribisha KMC FC jumatano (Oktoba 26) Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam katika mchezo wa Mzunguuko wa tisa, huku juma lijalo ikitarajiwa kupapatuana na Club Africain ya Tunisia kwenye mchezo wa Kombe la Shirikisho Hatua ya Mtoano.