Askofu Awaonya Wanaosaka Miujiza Makanisani




ASKOFU Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki Dar es Salaam, Thaddaeus Ruwa’ichi, amewataka wanawake nchini kutokubali kuyumbishwa na makanisa ya miujiza yanayoibuka kila kukicha.

Thaddaeus Ruwa’ichi.
Katika misa ya kilele cha Jubilee ya Miaka 50 ya Chama cha Kitume cha Wanawake Wakatoliki Tanzania (WAWATA) mkoani Dar es Salaam jana, Askofu Ruwa'ichi alisema ndani ya kanisa hilo hawajapungukiwa kwa kuwa kuna hazina zote za utakatifu wanaouhitaji kwa ajili ya wokovu.

“Zingatieni hazina mnayoipata ndani ya kanisa lenu Katoliki maana ni hazina kubwa, itafuteni hazina hiyo na muwe wajumbe wa kuipeleka kwa wengine,” alisema.

Askofu Ruwa'ichi alisema kuna tatizo kubwa linalowakabili kinamama wengi kwa sasa, sehemu kubwa wakiwa ni vijana na watoto wanaojilea wenyewe, akisisitiza kuwa 'ni hatari sana'.

“Ninaomba niwaangalishe kinamama, hiyo ni hatari na haina tofauti na yule anayelima shamba lake kisha haliangalii wala kulitunza, mwisho wa siku hutegemea kuvuna mabua, hivyo kinamama tafakarini hili la malezi,” alitoa angalizo.


Kiongozi huyo wa kiroho pia alisema anamshukuru Mungu kwa anayoyatenda ndani ya kanisa hilo kupitia kuwapo wanawake Wakatoliki.

“Pia tunamshukuru Mungu kuwa na kanisa lenye uhai wa vijana wengi, ambao zaidi ya asilimia 70 ni watoto na vijana, hii ni baraka, hivyo jukumu lenu kinamama kushirikiana na waume zenu kuhakikisha mnawapatia hawa watoto na vijana malezi ya imani na yenye maadili,” alisema.

Rais wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), Gervas Nyaisonga, alimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwaamini wanawake na kuwapa nafasi za kuongoza katika kada mbalimbali, huku akiomba radhi kwa niaba ya wanawake waoshindwa kufanya vizuri kwenye nafasi mbalimbali, akiamini wataendelea kufanya vizuri katika kujenga nchi.


“Ninawashukuru na kuwapongeza WAWATA na wanawake wote Tanzania, kwamba katika miaka yote 50 wameonyesha ujasiri, ustahimilivu na umakini mkubwa kukabiliana na shida ambazo nchi imezipitia kwa miaka yote. Katika nyakati zote wameonyesha umahiri mkubwa na ujasiri, wamekuwa sababu ya furaha na matumaini kwa Watanzania wote, ndiyo maana Tanzania inaendelea kushamiri,” alisema.

Askofu Nyaisonga alisema ukimwezesha mwanamke umeliwezesha taifa na wengi wanaamini kwenye karama hiyo.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad