MBUNGE wa Kawe kupitia Chama Cha Mapinduzi, Askofu Josephat Gwajima, ameibua gumzo baada ya kutangaza kufanya uteuzi wa wasaidizi wake wawili katika masuala ya michezo, utamaduni na sanaa. Anaripoti Mwandishi Wetu…(endelea)
Taarifa hiyo imetolewa leo Jumanne tarehe 25 Oktoba, 2022 na Victor Champoa ambaye ni Mkuu wa Kitengo cha Habari, Ofisi ya Mbunge wa jimbo la Kawe.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Gwajima ambaye pia ni Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima lenye makao yake makuu jijini Dar es Salaam, amemteua Ramadhan Kindamba kuwa msaidizi wake wa masuala ya Michezo, Utamaduni na Sanaa kata ya Mabwepande na Jamila Rajabu ameteuliwa katika wadhifa kama huo kwa Kata ya Bunju.
“Uteuzi unaanza mara moja,” ilieleza taarifa hiyo kwa umma.
Hata hivyo, taarifa hiyo imeibua gumzo katika mitandao ya kijamii ambapo wengi wameikosoa na wengine wakifanya kejeli.
Yericko Nyerere ni mmoja wao ambaye ameishirikisha taarifa hiyo katika ukurasa wake wa Twitter na kuandika msururu wa jumbe akikosoa hatua hiyo ya Gwajima.
“Daah (alama za kicheko) nchi ina ujinga mwingi sana aisee! kuna watu wanapenda mamlaka balaaa! Msaidieni Gwajima, ubunge sio cheo cha kimamlaka/udola. Ni cheo cha kisiasa cha kuhudumia umma tu kama kiunganishi cha wananchi na serikali, kigiriki wanaita ni demo-cratic-post,” ameandika Nyerere.
RamDan Gwataman @Ramdankg123 amejibu katika twitter ya Nyerere, “Sie wenye jimbo lake tunasubiria kwenda Marekani si aliahaidi! Huyu mzee mengine anayaingiliaje tena atuache na shida zetu bora hata yule Msaliti.”