KLABU ya Azam FC imesikitishwa sana na taarifa zinazoendelea kuenea kwenye Mitandao Mbalimbali ya ndani na nje ya Afrika, zikiihusisha Klabu hiyo na hujuma dhidi ya wapinzani wao katika CAF Confederation Cup, Klabu ya Al Akhdar SC ya nchini Libya.
Klabu hiyo imekanusha vikali kuhusika na jambo lolote baya dhidi wapinzani wake Al Akhdar SC, ikiamini kwamba chanzo cha tuhuma dhidi yake ni dhamira mbaya na ovu iliyolenga kuitoa mchezoni (mind games).
Yawezekana ni kweli kwamba Al Akhdar SC wamepatwa na changamoto za kiafya, jambo ambalo ni la kawaida kwa binadamu hasa anapobadili hali ya hewa…na tunawapa pole kwa hilo na kuwaombea kwa Mwenyezi Mungu awafanyie wepesi ili wapate nafuu mapema imesema taarifa kutoka Azam FC.
Aidha imefahamika kuwa Changamoto za kiafya kwa wachezaji wa Al Akhdar SC zilianza tangu wakiwa kwenye ndege kutoka kwao Libya kuja Tanzania.
Walipofika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere Dar Es Salaam, mchezaji wao mmoja alikuwa na hali mbaya kiafya na ikabidi achukuliwe na gari la wagonjwa kuwahishwa hospitali.
Kwa hiyo kuihusisha Azam y na changamoto zao za kiafya siyo jambo la kiungwana hata kidogo.
Sisi hatuhusiki na lolote kwa sababu hatukuwaandalia hoteli, hatuwaandalia chakula wala hatukuwa na ukaribu wowote nao, ambao ungeweza kumfanya mtu awe na shaka na sisi imeongeza taarifa hiyo kutoka Azam FC.