LICHA ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 nyumbani dhidi ya Al Akhdar ya Libya, Azam FC imeondoshwa rasmi kwenye Kombe la Shirikisho Afrika kutokana na tofauti ya mabao 3-2 baada ya kupoteza kwa kufungwa 3-0 ugenini siku chache zilizopita.
Azam yang'oka kibabe CAF
Katika mechi hiyo iliyopigwa leo usiku uwanja wa Azam Complex, matajiri hao wa Chamazi walihitaji ushindi wa mabao 4-0 ili kusonga mbele lakini imeshindikana na huenda wakajilaumu kutokana na wachezaji wake kutotumia vyema nafasi za mabao zilizotengenezwa.
Mabao ya Azam katika mchezo huo yalifungwa na Idris Mbombo dakika ya 27 akimalizia pasi mpenyezo ya Prince Dube na bao la pili lilikuwa la kujifunga kwa beki wa Akhdar dakika ya 58 katika hatua za kuokoa kwa kichwa mpira wa kutengwa uliopigwa na Ayoub Lyanga.
Sambamba na Azam kutolewa, timu nyingine kutoka Zanzibar, Kipanga imeondoshwa kwenye kombe la Shirikisho Afrika kwa jumla ya mabao 7-0 kutoka kwa Club Africain ya Tunisia.
Mchezo wa kwanza uliopigwa uwanja wa Amaan Zanzibar, ulimalizika kwa suluhu (0-0), na mabao yote saba yalifungwa jana kwenye mechi iliyopigwa Tunisia.