BANGALA: Sio beki tu, hata winga nacheza



UKIWEKA kando jina la Fiston Mayele staa mwingine ambaye amewapa heshima kubwa Yanga msimu uliopita ni kiraka Yanick Bangala Litombo, ambaye kazi ya miguu yake imeipa Yanga mafanikio makubwa kwa kuchukua mataji matatu lakini na yeye akiibuka kuwa Mchezaji Bora wa Ligi Kuu Bara msimu uliopita.

Bangala kwa ubora huo ukawafanya mashabiki kumpa jina la Mzee wa Kazi Chafu, hapendi kuongea sana lakini anafanya kazi kwa ubora sana. Ubora huo ukalifanya Mwanaspoti kufanya naye mahojiano maalum akielezea safari yake ya soka hadi kutua Yanga na hadi mafanikio ndani ya mabingwa hao wa Ligi Kuu Tanzania.

SOKA TANZANIA

Bangala anaeleza tofauti ya soka la Tanzania na kwingineko alikopita akisema:

“Ligi ya Tanzania ni nzuri. Mpangilio uko vizuri kabisa, dosari ni ndogo, hakuna mabadiliko makubwa sana ya ratiba ya mechi, ukiona mechi imepangwa tarehe fulani, basi asilimia kubwa inachezwa. Kidogo kuna changamoto ya viwanja lakini wanajitahidi sana sasa kuhakikisha vinakuwa bora ,”anasema Bangala huku akifichua juu ya uamuzi wake wa kujiung na Yanga kwa kusema; “Wakati naamua kuja kucheza Yanga, nilikuwa naona ni uamuzi sahihi kwangu. Mimi ni mchezaji mpira, nikasema sasa nakwenda Tanzania na sikuona kama ni uamuzi mbaya kwa kuwa nilijua ni aina gani ya klabu ambayo nakwenda kuitumikia.”


MATATU MSIMU MMOJA

Msimu wake wa kwanza tu akiwa na Yanga Bangala anakuwa mmoja kati ya mastaa ambao waliishuhudia timu hiyo kongwe ikirejesha hadhi yake ya mataji ikichukua makombe matatu. Anaeleza jinsi msimu ulivyokuwa.

“Wakati nakuja Yanga ilikuwa furaha kubwa kwangu, kwa sababu kuna wachezaji wengi walisajiliwa hapa wakati nafika, ambao nilikuwa nao AS Vita ya kule kwetu, hawa ni wachezaji ambao wananijua na nawajua, niliwaacha kwa mwaka mmoja tu pale nilipojiunga na FAR Rabat kule Morocco.

“Nilipofika hapa nilikuta tunatakiwa kuweka nguvu kuchukua mataji na uwepo wa hawa wachezaji wenzangu na wengine ambao tuliwakuta ulitupa wepesi wa kufanikisha malengo yetu. Hatua ya kwanza ikawa ni kuchukua Ngao ya Jamii, tulipoifunga Simba tukaweza kwenye akili yetu kwamba kila kitu kinawezekana na Mungu akatuwekea wepesi tukafanikisha zaidi kuchukua makombe mengine.”


SIRI YA UBORA

“Sio kama ligi ya hapa ni nyepesi, sio kweli, nilianza soka nikiwa kijana mdogo sana, nikiwa na kipaji, wazazi wangu hawakunizuia kucheza soka, nilianza kuchezea Timu za Vijana za Taifa wadogo kabisa kule DR Congo kuanzia chini ya umri wa miaka 17, 20, 23 nikaenda mpaka timu kubwa ya taifa, baadaye nikaenda kucheza sehemu nyingine duniani, huko niliongeza uzoefu mkubwa, nimecheza mechi nyingi mpaka nafika hapa Yanga, ndio maana nikiwa uwanjani nashirikiana vizuri na wenzangu, kifupi ni uzoefu nilionao, unanipa hali ya kujiamini sana kwa kuwa kipaji ninacho.”


KILICHOMTOA RABAT

Kabla ya kuja Yanga, Bangala alitokea FAR Rabat ya nchini Morocco iliyokuwa inafundishwa na kocha wa zamani wa Simba, Sven Vandenbroeck, hapa anaeleza sababu iliyomfanya aikimbie timu hiyo.

“Nikiwa FAR Rabat mambo yalikuwa vizuri wakati nafika Morocco kocha ambaye nilimkuta alikuwa ananitumia kama kiungo namba sita nikianza kikosi cha kwanza nikicheza mechi zote vizuri, baadaye yule kocha wakamuondoa na kumleta Sven. Akaniona ninavyocheza akasema hapana kwa kuwa anataka soka la kuanza kucheza kuanzia nyuma mpaka mbele.

“Alipoona ubora wangu Sven akanirudisha nyuma kucheza kama beki wa kati ili tucheze soka analotaka kwa kuwa nina uwezo wa kuanza kuchezesha timu kuanzia nyuma na kukaba vizuri, shida ikaja Rais wa ile klabu kulikuwa na mchezaji wake anampenda sana na alikuwa anacheza beki wa kati, sasa mimi niliporidishwa kucheza beki yule mchezaji wa rais wa klabu akawa hana nafasi.


“Rais akamfuata kocha na kumtaka awe anafanya mzunguko wa nafasi leo nicheze mimi na wakati mwingine acheze beki wake anayemtaka. Sikupenda ile, huwa nataka nikienda klabu yoyote nicheze kwa kuwa nina uwezo, nikamfuata Kocha Sven nikamuuliza kulikoni, akaniambia mwenye timu ametaka hivyo.

“Sikufurahia hiyo hali niliwafuata viongozi na kuwaambia ni bora nivunje mkataba niondoke, unajua shida yangu nyingine ilikuwa mkataba wangu ambao ulikuwa unanitaka kila ninapocheza mechi nyingi pia pesa yangu inaongezeka.

“Yale mabadiliko ya kuwa nacheza leo kesho sichezi yalisababisha kupungua zile mechi na kupungua huko kungenifanya pia pesa nilizotakiwa kupata zisingefikia.

“Nikaona uamuzi sahihi ni kuondoka tu hapo, wakati nawaambia nataka kuondoka viongozi wengine wa klabu hawakupenda kabisa wakinitaka nibaki lakini bahati mbaya nilishafanya maamuzi, sababu kubwa ya kunitaka kubaki ni kwamba wakati nafika FAR Rabat ilikuwa imepita muda mrefu hawajawahi kushiriki mashindano ya Afrika badaaye niliwasaidia kurudi katika mashindano hayo.”


ISHU NA SVEN

“Hata nilipofika hapa Yanga baadhi ya viongozi wa FAR Rabbat waliendelea kunisumbua nirudi kwa kuwa waliyumba sana baada ya kuondoka, nisingeweza kurudi tena, niseme ukweli sikuwa na shida kabisa na Kocha Sven, nawasiliana naye sana mpaka sasa nikiwa hapa Yanga na yeye akiwa Qatar, anafuatilia mpaka mechi za ligi ya hapa anaangalia ninavyocheza ananishauri niboreshe kipi, hata nikicheza vibaya ananikosoa na kunijenga.”

KUMBE NI WINGA

Bangala anajulikana kwa sifa kubwa kwamba ni kiraka, akiwa na uwezo wa kucheza nafasi nyingi. Hapa anaeleza kwa undani juu ya nafasi ambazo anaweza kuzicheza uwanjani kwa ufasaha.

“Wakati naanza kucheza soka nilikuwa nacheza nafasi ya winga wa pande zote mbili, baadaye nikabadilishwa kuja kucheza beki na naweza kucheza beki zote kule nyuma lakini pia naweza kucheza nafasi zote za kiungo wa kati kaunzia mkabaji mpaka mchezeshaji, nakumbuka wakati nikiwa AS Vita tulikuwa tukikutana na timu za kutoka Uarabuni, kocha Ibenge (Florent) alikuwa ananichezesha kama namba 10 ili tuanzie kukaba kuanzia juu.

“Kwa sasa siwezi tena kucheza kama winga nimeshasahau vile vitu vitu vitakavyonifanya nionekane bora kama zamani, ila ukinipanga kuanzia namba kumi kurudi nyuma naweza kucheza vizuri tu bila shida yoyote.”

NAFASI SAHIHI

“Nakuwa na furaha sana kama kocha atanitaka kucheza kama kiungo mkabaji, nikicheza hapo nakuwa na amani sana na watu watafurahia kazi. Huo ni uamuzi wa kocha anipange wapi kama beki lakini kama ni uamuzi wangu basi ni kucheza kama kiungo mkabaji,” anasema Bangala ambaye amefichua pia ishu yake ya kuonekana kuzozana mara kadhaa na Kipa Diarra Djigui na kufafanua:

“Hapana hatuna ugomvi na Diarra tuko sawa kabisa, ile huwa inakuwa ni kuelekezana uwanjani tunapoona mambo hayako sawa, sisi ni binadamu naweza kukosea mimi au yeye (Diara) au mchezaji mwenzetu mwingine yoyote.

“Anaweza kunifuata na kuniambia Yannick hapa ulikosea ulitakiwa kucheza hivi, naye akifanya kosa naweza kumwambia huwa tunaelekezana tu unajua kila mchezaji uwanjani ana umuhimu wake. Diarra anaweza kunifuata na kuniambia tunashambuliwa sana waambie wale wa juu waanzie kukabia kulekule, hatuwezi kucheza kama mabubu ni lazima tuongee kukumbushana hakuna shida yoyote tuko sawasawa.”

TUZO YA TPL

Bangala anasema hakutarajia kupata Tuzo ya Mchezaji Bora wa Ligi Kuu Tanzania.

“Sikutarajia kupata heshima hii ya kuwa, akilini kwangu ilikuwa nakuja Yanga ili ichukue ubingwa wa hapa ambao ni muda haukuwepo, nilichopanga ni kuipigania klabu yangu kwa heshima waliyonipa ya kuja kuitumikia lakini ndani ya kazi hiyo kumbe uwezo wangu pia ulitambulika. Kwangu ilikuwa kama sapraizi kupata tuzo sikutarajia kabisa, hii ni heshima kwa klabu mashabiki na wachezaji wenzangu, sichezi ili nipate tuzo kitu cha muhimu kwangu ni timu.

Bangala anasema anashukuru msimu huu umeanza vizuri na watapambana lakini hakuna anayejua watapata mafanikio gani mwisho wa msimu.

‘Lakini kubwa tuna malengo na tunataka kuweka nguvu kubwa tufike hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika. Tumeambiwa mara ya mwisho ilikuwa mwaka 1998 tunataka kurudi katika hatua hiyo na zaidi.”

HAPENDI KUPOTEZA DABI

Kama hujui Bangala ndiye mchezaji ambaye huwa anawaimiza sana wenzake kuhakikisha wanashinda wakati wanaingia uwanjani na hata wanapokuwa ndani ya uwanja hapa anaeleza

“Kwanza niseme huwa sipendi kupoteza mechi ya watani, hii nimetoka nayo Congo nakumbuka hata nilipokuwa mdogo nilikuwa naona upinzani wa AS Vita na DC Motema Pembe ile ikanijenga zaidi.

“Nilipofika hapa nikakutana na hii ya Simba na Yanga, hivyo hakuna kipya huwa naendelea na nidhamu yangu ileile, huwa nawaambia wenzangu tusikubali kupoteza hii mechi kubwa, unajua mchezaji mkubwa anaonekana kwenye mechi kubwa, mfano mechi ya Simba iliyopita, wakati tunamaliza kipindi cha kwanza tulipofika vyumbani mapumziko nilimfuata mdogo wangu Fiston (Mayele), nikamwambia hakucheza vizuri dakika 45 huwa hatuchezi vile mechi ya watani.

“Nikamwambia abadilike haraka, hakuna beki wa kumuweza pale Simba, atulize presha na anaweza kuwafunga Simba hata zaidi ya mabao mawili na kweli aliporudi alibadilika na akafunga mabao mawili, unajua Mayele ni kati ya wachezaji bora sana tulionao.”

RASTA UWANJANI

Akiwa uwanjani Bangala huwa na mwonekano wa nywele zake zilizosukwa kwa kwenda nyuma lakini nje ya uwanja kuna Bangala mwingine anayevaa kofia fulani za kisasa hapa anaeleza.

“Kofia ni staili yangu, hapa napenda sana kuvaa kofia kutokana na jua kali, unajua kuna wakati natakiwa kutembea sehemu huwa sipendi watu wanisumbue ila ninaporudi nyumbani huwa nakuwa kawaida tu bila kofia.”

Anasema yeye ni mtu wa kupiga pamba sana. “Unajua sisi Wakongomani tunapenda kuonekana nadhifu, tumevaa nguo nzuri na nguo nzuri zina gharama sana, ni kweli natumia fedha nyingi katika kutafuta nguo nzuri, hata kofia kama nikikutana nayo nzuri nimeipenda nainunua, siwezi kusema natenga bajeti kwa ajili ya nguo hapana.


ANASUKWA NA MKE

“Kuhusu hizi nywele zangu huwa nasuka nyumbani kama mkewangu anakuwepo ingawa kuna wakati nakwenda saluni, nikiwa Congo niliwahi kutumia mtindo mwingine lakini hapa niliamua mtindo wangu wa nywele uwe huu kwa kuwa umeshazoeleka hapa.”

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad