WAKATI Yanga wakiumiza vichwa kutoboa hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika, beki wa zamani wa Simba, Amri Said ‘Stam’ ameipa maujanja timu hiyo namna ya kuwakabili Al Hilal katika mchezo wa marudio.
Yanga inasuka mipango kupata matokeo mazuri dhidi ya wapinzani hao baada ya mechi ya kwanza kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa kulazimishwa sare ya bao 1-1 na sasa inahitaji ushindi au sare kuanzia mabao mawili ili kujihakikishia nafasi.
Timu hizo zinatarajia kurudiana Jumapili huko Sudan na mashabiki na wadau wa soka nchini wakitofautiana mtazamo baadhi wanaipa matumaini Yanga kufuzu na wengine wakiamuachia Mungu.
Akizungumza na Mwanaspoti, Stam alisema kazi kubwa ipo kwa Kocha wa Yanga, Nasreddine Nabi kuwaandaa nyota wake kiakili, maarifa na mbinu mpya kwani mchezo huo unaweza kuwa rahisi kutoboa.
Alisema ili waweze kufanya vizuri lazima Kocha Nabi awapange vizuri vijana wake, hasa upande wa mabeki Kibwana Shomari na Masoud Djuma wasishambulie kama mchezo uliopita.
“Mabeki wanne wanabaki nyuma, pembeni Benard Morrison na Jesus Moloko huku katikati Salum Aboubakari, Feisal Salum na Khalid Aucho ambao watapeleka mashambulizi mbele kuwakuta kina Aziz KI na Fiston Mayele,” alisema Stam.
Beki huyo ambaye kwa sasa ni Kocha Mkuu wa KVZ ya Zanzibar aliongeza katika mechi hiyo Yanga isiende kupaki basi, bali iwapelekee moto Al Hilal mwanzo mwisho itafanikiwa.
Alisema Nabi anapaswa kwenda na uamuzi mgumu kama alivyofanya mpinzani wake, Kocha wa Al Hilal, Florent Ibenge kuzuia hatari kutoka kwa mawinga wake na kuwapa ugumu nyota wa Yanga.
“Naiona bado Yanga ikienda na mipango ya kushambulia lakini ikatuliza akili bila presha, wanaweza kufanikiwa. Ugumu pia upo kwakuwa wale wapo nyumbani na bao lao la ugenini linawapa nguvu kujiamini,” alisema kocha huyo bora wa mwezi Septemba Ligi Kuu Zanzibar.