Bima ya Afya Sh 84,000 mtu mmoja kwa mwaka



KIWANGO cha kujiunga na Bima ya Afya kwa wote kwa wale ambao hawana familia ni  kiasi cha Sh 84,000 kwa mtu mmoja kwa mwaka, ambayo ni sawa na wastani wa Sh 7,000 kwa mwezi.

Kwa kaya ya watu sita itakuwa Sh 340,000,  akiwemo mchangiaji, mwenza wake na wategemezi wasiozidi wanne kwa mwaka, pindi sheria hiyo itakapojadiliwa na kupitishwa bungeni.

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Prof. Abel Makubi leo, wakati wa kikao na Wakurugenzi wa Wizara na taasisi zilizo chini ya Wizara ya Afya, kuhusu sheria ya Bima ya Afya kwa wote kilichofanyika katika Hospitali ya Benjamin Mkapa jijini Dodoma.

Prof. Makubi amebainisha kuwa kwa wananchi watakaotambuliwa kutokuwa na uwezo, wataendelea kupatiwa huduma kwa utaratibu utakaowekwa na serikali kwa kila mtu kuwa na kadi yake ya Bima ya Afya.


“TASAF na mifumo ya maendeleo ya jamii ndio itakayofanya utambuzi kwa wananchi wasio na uwezo, ili kuiwezesha serikali kuweka utaratibu madhubuti wa kutoa huduma kwa wananchi wasio na uwezo kupata huduma, pindi wanapohitaji,” amesema Prof. Makubi.

Pia Prof. Makubi ameweka wazi kuwa endapo sheria itapitishwa, basi wizara imejipanga kuanza mara moja utekelezaji wa sheria hiyo bila kikwazo ifikapo Julai 1, 2023, kwani suala hilo sio la ghafla.

“Suala la sheria ya bima ya afya kwa wote sio dharura limefanyiwa mchakato kwa muda mrefu zaidi ya miaka 10, kwa ushirikishi mkubwa wa wadau,” amesema Prof. Makubi.


Muswada wa sheria hiyo ulisomwa kwa mara ya kwanza katika Bunge Septemba 27, 2022
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad