CHADEMA YAJA NA MAPYA KUHUSU KIKOSI KAZI




Dar es Salaam. Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika ameitaka Serikali kuweka wazi gharama ambazo kikosi kazi kimetumia huku akisema hakukuwa na haja ya kuundwa kwa kikosi hicho kwa sababu kazi ya kutafuta maoni ya wananchi ilifanywa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyoongozwa na Jaji Joseph Warioba.

Mnyika ameeleza hayo leo Jumamosi Oktoba 22, 2022 Jijini Dar es Salaam ikiwa ni siku moja baada ya kikosi kazi cha kuratibu maoni ya wananchi kuhusu demokrasia ya vyama vingi, kukabidhi ripoti yake kwa Rais Samia Suluhu Hassan.

Katika ripoti hiyo, kikosi kazi kimetoa mapendekezo 18 kwa Serikali ikiwemo kuruhusiwa kwa mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa, mchakato wa katiba mpya kuendelezwa na ruzuku kwa vyama vyote vya siasa.

Hata hivyo, Rais Samia alitoa angalizo kwamba mapendekezo hayo siyo amri kwa Serikali kuyatekeleza. Alisisitiza kwamba wameyapokea na watayafanyia kazi hasa yale ambayo hayahusishi mabadiliko ya sheria.


Akizungumza na vyombo vya habari, Mnyika amesema kikosi kazi hicho kiliundwa ili kuchelewesha mchakato wa katiba mpya na kwamba hilo limejidhihirisha kwenye mapendekezo waliyoyatoa.

Amesema maoni ya wananchi yalikusanywa na Tume ya Warioba, hivyo hakukuwa na haja ya kuundwa kwa kikosi kazi, bali wangerejea kwenye kitabu cha maoni ya wananchi kilichoandaliwa na Tume ya Warioba.

"Kuundwa kwa kikosi kazi ni matumizi mabaya ya fedha za Watanzania. Tunaitaka Serikali itoke hadharani ituambie kikosi kazi kimetumia fedha kiasi gani," amesema Mnyika.


Amesema walikuwa wakipigania kuruhusiwa mikutano ya hadhara lakini baada ya kuundwa kwa kikosi kazi waliamua kukipa muda ili waone matokeo yake, lakini wameshangazwa na kauli ya Rais Samia wakati akijibu hoja hiyo akisema kuna haja ya kufanyia mabadiliko sheria na kanuni kabla mikutano haijaruhusiwa.

"Tunaitaka Serikali iruhusu mikutano ya hadhara bila kusubiri mabadiliko ya Sheria ya Vyama vya Siasa, bila kusubiri mabadiliko ya kanuni za mwaka 2019, bila kusubiri mabadiliko ya Sheria ya Jeshi la Polisi.

"Zuio la mikutano ya hadhara ni haramu kwa sababu liko kinyume na Katiba ya nchi, liko kinyume na Sheria ya Vyama vya Siasa," amesema Mnyika.

Amesema wameshangazwa na kauli ya Rais Samia kwamba mapendekezo ya kikosi kazi siyo amri kwa Serikali, huku akisisitiza kwamba wanataka kujua gharama zilizotumiwa na kikosi kazi.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad